Usalama wa wanahabari Tanzania uko mashakani

Muktasari:

  • Kwa nini inaweza kuja kwa mtu yeyote anayehitaji kufahamu, lakini mbele ya swali hilo na majibu yatakayotokana na swali lenyewe, vinaweza kuzalisha maswali mengine lukuki.

Kwa nini? Hilo ni swali gumu kulijibu kwa mtu yeyote kama atakutana nalo na mara nyingi muuliza swali hutakiwa kujipanga ili kulitengeneza swali hilo.

Kwa nini inaweza kuja kwa mtu yeyote anayehitaji kufahamu, lakini mbele ya swali hilo na majibu yatakayotokana na swali lenyewe, vinaweza kuzalisha maswali mengine lukuki.

Kwa mfano, unapouliza kwa nini unataka au unatarajia kupokea nini, kwa nani, ili iweje, wewe utafaidika na nini. Na ikiwa uliuliza kwa sauti, hao waliosikia watafaidika na kitu gani.

Hivi karibuni tasnia ya habari nchini ilitikiswa kwa kuondokewa na vijana wake mahiri.

Hapa narejea ajali za barabarani zilizotokea mikoa ya Arusha na Geita na kuacha msiba mzito kwa wanahabari na familia za husika za marehemu. Ni wanahabari waliokufa wakiwa kwenye majukumu yao ya kihabari

Nimechukua muda mrefu kujiuliza swali hilo la kwa nini? Sijapata majibu. Nimeendelea kujiuliza maswali tena na tena ya kwa nini na itaendelea kuwa kwa nini mpaka majibu yapatikane kwa wakati unaotakiwa.

Hivi kuna wakati umewahi kujiuliza kuhusu matukio ya vifo vya waandishi katika ajali?

Je, umejiuliza kuhusu ajali mbaya zilizotokea katika msafara wa kiongozi mmoja katika kanda ya Ziwa, ambako mara mbili magari ya waandishi yalipata ajali. Kwa nini iwe kwao? Madereva walikuwa wazembe au magari yalikuwa na hitilafu?

Alikufa Shadrack Sagati kule Geita akiwa katika msafara wa maofisa wa Wizara ya Viwanda na Biashara, akafa Hamza Temba akiwa katika safari pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii,

baadaye yakaja magari yaliyowabeba waandishi kwenye msafara wa kiongozi mmoja aliyekuwa katika ziara zake maeneo mbalimbali ya kanda ya Ziwa. Ingawa hawa hawakufa, lakini wamebaki na maumivu.

Unaweza kusema, kifo ni mpango wa Mungu ambao uamuzi wa kumchukua mtu hutegemea na kalenda aliyompangia na sote tunaamini hivyo.

Lakini tunajiuliza ni kwa nini kwa waandishi pekee? Mko katika msafara au ndani ya chombo kimoja anakufa mmoja na mwingine anabaki na kesho inakuwa hivyohivyo.

Cha msingi hapa ni kujua, hivi waandishi wanakaa wapi wanapokuwa kwenye magari ya viongozi, usalama wao uko wapi, nani anawataka kukaa hivyo, kwani wakigoma itakuwaje au nini kitatokea?

Wengi tuliomo katika taaluma hii tunaweza kukubaliana kuwa, waandishi wanakaa katika viti vya nyuma ambavyo mara nyingi huwa hakuna ulazima au hakuna kabisa mikanda ya kufunga kwa ajili ya usalama wao.

Watu wa aina hiyo ikitokea ajali wanakuwa katika kipindi kigumu zaidi kujiokoa na hujikuta wakipata majeraha makubwa au kusababisha vifo kama ilivyotokea hivi karibuni kwa wenzetu.

Waandishi hufananishwa na watu wa ziada kwenye misafara hiyo, kwani mara kadhaa tunashuhudia hata maofisa wa Serikali wanaposafiri, pindi wapatapo watu wa kuwasaidia katika magari yao, lazima mwandishi ahamishiwe kiti cha nyuma.

Kiongozi akiwa na ndugu yake au msaidizi wake na ndani yake ukawepo mwandishi wa habari, wewe utaambiwa ‘mpishe hapo wewe mzoefu kaa nyuma.’

Kama hiyo haitoshi, kwenye misafara mikubwa waandishi watapewa magari yaliyochoka huku wakiwekwa nyuma ya msafara.

Cha ajabu mwenye msafara akitaka kuzungumza na watu, waandishi huwa wa kwanza kuitwa ili kusikia matamko na maagizo!

Kwa nini inakuwa hivyo? Kwa nini kada hii inakosa inachostahili hata kuwafanya wapaza sauti hawa kuwa na mashaka na hofu kila wanapotembea katika majukumu yao?

Hivi ni kwa nini wao kila siku wawekwe kwenye magari mabovu? Kwa nini wao wawekwe nyuma kila gari wanalopanda katika misafara ya viongozi?

Nani anaweza kuiona hali hiyo ili kuwasaidia waandishi ambao umuhimu wao ni mkubwa kwa jamii na Taifa kwa jumla?

Huu ni wakati wa kuwa na mjadala mrefu ama wa kitaifa ili kulijadili jambo hili, kwa maana ya kuwaondolea hofu ambayo imeanza kutawala katika fikra za waandishi.

Kikubwa kuinachotakiwa ni kuona njia bora ya kufanya ili kwenye misafara watu hawa wawe na hadhi sawa na wengine, huku wakipewa usafiri wa uhakika, badala ya kuonekana kama watu wa kupewa fadhila tu ya usafiri. Kama hayo yatafanyika, sina shaka swali la kwa nini litakuwa limepungua ukali wake na linaweza kuja pale inapolazimu tu na si vingine.

Waandishi nao wajisaili. Wanapaswa kubadilika. Lazima watetee uhai wao kwa kila hali. Uhai wako ni zaidi kuliko habari unayoitafuta.

Habel Chidawali ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Dodoma. [email protected]