Usaliti huu wa kisiasa mnajenga mnabomoa?

Saturday March 16 2019Kalunde  Jamal

Kalunde  Jamal 

By Kalunde Jamal

Siasa imekuwapo miaka mingi nyuma na waasisi wake waliamini kuwa vijana ndiyo watalizungusha ipasavyo gurudumu hilo.

Sababu za wao kufanya hivyo au kuaminiwa kuwa wanaweza kuliendesha vyema gurudumu hilo inatokana na nguvu walizonazo za kukabiliana na changamoto na mikikimikiki ya siasa.

Hata 1992 Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi iliporidhia kurudisha tena mfumo wa vhama vingi hapa nchini walikuwa wahamasishaji wa siasa, ikiwamo kujiunga na vyama vingine mbali ya CCM iliyokuwa madarakani ili kuleta mapinduzi ya kimtazamo kwa kuviunga mkono, wengi wao walikuwa vijana.

Baadhi ya vijana walionyesha kukomaa kifikra na kimtizamo katika hatua zile za awali ambazo wazazi, familia, marafiki na jamii kwa ujumla isengekuwa rahisi kuwaelewa kwa sababu bado kulikuwa na homa iliyogubikwa na woga wa kukubali mfumo wa vyama vingi.

Licha ya wakubwa zao kuanzisha vyama vya upinzani au wale walioasisi CCM, bado walihitaji nguvu ya vijana kuhakikisha chama na dhamira ya vyama vingi inatambulika nchi nzima, huku kila mmoja akizunguka kukinadi chama chake kuwa ndicho cha kweli na kitamletea Mtanzania mafanikio ya moja kwa moja.

Hili lilikuwa ni suala la kijasiri na lililoonyesha waziwazi umuhimu wa vijana wenye fikra pevu.

Miaka ya hivi karibuni uelewa wa vijana kwenye masuala ya siasa umekuwa mkubwa kutokana na asasi za kiraia kutoa elimu mijini na vijijini.

Hii imewasaidia wenye nia njema kujifunza zaidi na kubishana kwa hoja, wengine wakijenga hoja madhubuti na kuwavutia wenzao walio upande mwingine kujiunga nao. Huu bila shaka ni ushindi na si kitu kinachopaswa kubezwa hata kidogo.

Hata hivyo kila mazuri yana mabaya na hasara zake, ndivyo ilivyo kwa siasa za vijana kwani elimu ya kujua jambo hili badala ya kuwakuza inawadumaza.

Kadri uelewa unavyokuwa juu ya siasa ndivyo vijana wanavyoshindwa kusimamia wanachokiamini na badala yake wanayumbishwa.

Yamekuwa yakisemwa mambo mengi kuhusu vijana na wanachama kutoka chama kimoja kwenda kingine ikiwamo kununuliwa (sina hakika na hilo) au kufuata mkumbo, wanataka madaraka na kwa baadhi ya haya yanayosemwa yanaonekana wazi na kufanya kijana apoteze umakini katika kuamua.

Badala yake wamekuwa kama hawaelewi wanatakiwa kufanya nini, wengi wamejiingiza kwenye makundi ya kiuanaharakati kisiasa na kujikuta wakiambulia kutumika.

Walianza vizuri wakiwa na lengo moja la kukuza siasa za upinzani wa hoja, kupigania hali zao kupitia demokrasia, kupigania wanachokiamini, lakini sasa wanapaza sauti ili wasikike waitwe mahali kwa ajili ya kunufaisha wengine.

Tabia hii ndiyo baadhi ya watu katika jamii wameipachika jina la “umalaya wa kisiasa” ambapo badala ya kujikomaza na kujifunza zaidi kupitia wimbi la siasa linaloendelea nchini , vijana wengi wamekubali liwakumbe na kuwapeleka wasipopajua.

Haiwezekani kijana ndani ya muhula wa miaka mitano uwe umejiunga na vyama vitatu au umehama vyama mara tatu, huko ni kuyumba na kutojua unatakiwa kufanya nini.

Kuyumba huku kisiasa kumewafanya baadhi ya vijana kuwa ‘mavuvuzela’ wa kupiga kelele, kuhubiri wasichokitaka bali kinachotakiwa na wanaowafanyia maamuzi.

Hii imesababisha kipindi fulani vijana wanashindwa kueleweka ndani ya jamii kutokana na matendo, kauli wanazozitoa kubadilika badilika kila baada ya muda.

Wengi pia hawaeleweki wapo upande gani, kwa sababu badala ya kuunga mkono sera ambazo zinakibeba chama fulani baadhi yao humuunga mkono mtu au kile wanachokitegemea kukipata kwenye huo upande wanaouunga mkono.

Hapa dhamira ya kujikita kwenye siasa inabadilika kutoka kwenye ukombozi na kutafuta mabadiliko kwa njia ya demokrasi, inakuwa ni kwa maslahi na matakwa ya pande mbili - anayefanyiwa uamuzi na aliyekubali kufanyiwa uamuzi kwa sababu fulani fulani. Kumbuka kijana ni Taifa linaloendelea, hivyo akiyumba katika uamuzi Taifa lijalo litayumba pia kwa sababu litakuwa linaongozwa na chembechembe ya kizazi kisichokuwa na dira.

Inafahamika wazi kuwa vijana ndio chachu ya mabadiliko. Ukweli wa usemi huu unadhihirika pale ambapo vikundi mbalimbali vya kisiasa, kidini na vya kijamii kuonekana kuwatumia vijana katika harakati zao, lakini kwa mwenendo wa siasa za sasa vijana wanaonyesha kushindwa na kujikuta wakitangatanga.

Kutangatanga huku na kuzurura kisiasa kunazalisha wanasiasa vijana wasioelewa wanataka nini, mabadiliko, demokrasi au kuwa bidhaa inayosubiri kutumika kwa masilahi fulani. Naam. Wanasiasa vijana hasa nyakati kama hizi kuelekea uchaguzi badilikeni. Tokeni mliko, piganieni maisha ya wananchi.