MAONI: Uwanja wa Ndani wa Taifa uboreshwe

Monday May 20 2019

Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA), inaendelea Uwanja wa Ndani ya Taifa, Dar es Salaam.

Michuano hiyo inayofanyika kila mwishoni mwa wiki, inashirikisha timu za mkoa wa Dar es Salaam na wachezaji wanaofanya vyema wanapata fursa ya kuitwa kwenye timu ya Taifa.

Mchezo wa mpira wa kikapu nchini ni maarufu na katika miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, ulipokewa vyema na idadi kubwa ya mashabiki.

Ingawa soka itabaki kuwa namba moja, lakini mpira wa kikapu ulipata umaarufu na kuiweka kando michezo mingine kama riadha, ngumi na netiboli.

Mpira wa kikapu uliwahi kuitangaza Tanzania kimataifa kutokana na viwango bora vya wachezaji wetu ambao walizipiku nchi jirani za Afrika Mashariki na Kati.

Dar es Salaam ndio mkoa unaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wa viwango bora kulinganisha na mikoa mingine ambayo mchezo huo si umaarufu.

Advertisement

Itakumbukwa mchezo huo ulishika hatamu wakati huo Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (BD) kikiongozwa na mwenyekiti Simon Msofe na katibu Mbamba Uswege ambaye sasa ni marehemu.

Viongozi hawa walifanya kazi kubwa ya kuutangaza mchezo huo na haikuwa ajabu kutoa baadhi ya wachezaji kucheza mpira wa kikapu nje ya nchi mfano ni Abdallah Ramadhani ‘Dulla’, Atiki Matata na Shaban Kazumba, kutaja wachache.

Hata hivyo, pamoja na umaarufu wa mchezo huo Dar es Salaam, miundombinu ya Uwanja wa Ndani, imekuwa si rafiki kwa muda mrefu.

Uwanja huo ambao pia umekuwa ukitumika kwa mashindano ya kimataifa ya Afrika ya michezo ya ndani, umekosa sifa kutokana na miundombinu yake kutokuwa rafiki. Hamasa ya mashindano ya kikapu imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na idadi ndogo ya mashabiki wanaojitokeza kwenda uwanjani hapo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuhofia kunyeshewa na mvua zinazoendelea.

Kwa mfano, katika mechi zinazoendelea hivi sasa, mara kwa mara waamuzi wamekuwa wakilazimika kusimamisha mchezo kwa muda ili kutoa nafasi kwa wasimamizi kupiga deki kuondoa maji yaliyosababishwa na mvua hivyo kuondoa ladha ya mchezo.

Mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zimekuwa kikwazo kwa wachezaji wa timu hizo kuonyesha viwango vyao uwanjani.

Kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikitoa ahadi ya kujenga upya uwanja huo, lakini hadi sasa ahadi hiyo haijatekelezwa licha ya miundombinu yake kuendelea kuwa mibovu.

Wakati umefika Serikali kuutupia jicho Uwanja wa Ndani na kuufanyia marekebisho ya kina ili kutoa fursa kwa michuano mbalimbali kufanyika.

Kwa kuwa uwanja huo ndio kitovu cha kuzalishwa idadi kubwa ya wachezaji, ni vyema marekebisho hayo yakafanyika haraka.

Tunaamini uwanja huo ukifanyiwa maboresho unaweza kuwa sababu mojawapo ya kuinua hamasa ya mpira wa kikapu na michezo mingine ya ndani na kupata timu bora za Taifa kwani licha ya wachezaji kuonyesha viwango, mashabiki watajitokeza kwa wingi kwenda kushuhudia timu zao zikishindana.