Vijue vigezo sita vya kukupa ajira

Muktasari:

  • Kuna vigezo kadhaa wanavyotumia waajiri kuajiri ikiwamo ubunifu,  uwezo wa kuongoza wengine,  namna ya unavyohusiana na wengine, nidhamu yakazi, mawasiliano bora na uzoefu.

Katika makala yaliyopita, tuliona takwimu zinazothibitisha kuwa tatizo la ajira ni zaidi ya kukosekana kwa nafasi za kazi.

Ingawa watafuta kazi wengi hufanya juhudi za kuthibitisha kuwa wanao ujuzi rasmi waliousomea darasani, siyo waajiri wengi wanathamini alama za darasani zinazoonekana kwenye vyeti vya waombaji hao.

Badala yake, mwajiri kwa kawaida hutafuta ujuzi ambao mara nyingi mtafuta kazi hautegemei.

Ujuzi huo, tulioupachika jina la ‘ujuzi mwepesi’, ni pamoja na ule uwezo wa kutumia maarifa ya jumla ya darasani katika kutatua matatizo halisi yanayomkabili mwajiri katika eneo lake la kazi.

Waajiri wanatafuta ujuzi ambao si mara nyingi hupatikana darasani, ndio sababu matangazo mengi ya nafasi za kazi hayaweki msisitizo mkubwa katika sifa za kitaaluma anazohitajika kuwa nazo mwomba kazi bali ‘ujuzi mwepesi’ tutakaoujadili katika makala haya.

Je, mwajiri hutarajia ujuzi gani kwa mwombaji wa kazi? Tutazame mifano michache.

Ubunifu

Mwajiri mzuri anategemea kuona namna gani mwajiriwa anaweza kufikiri nje ya mazoea. Huu ni uwezo wa kufikiria majibu yasiyozoeleka ya changamoto zilizopo ili kuongeza ufanisi wa kazi. Ubunifu ni pamoja na namna mwajiriwa anavyoweza kutumia rasilimali chache zilizopo kuleta matokeo yanayozidi matarajio.

Kwa mfano, unapoweza kutumia Sh 100 kuleta matokeo yaleyale ambayo yangeweza kuletwa kwa kutumia Sh 1,000, hapo unakuwa umelazimika kufikiri nje ya sanduku la mazoea.

Kwa kuwa umeweza kutumia rasilimali kidogo kuleta matokeo makubwa, unakuwa umemnufaisha mwajiri wako, jambo ambalo kwa hakika ni kipaumbele kikuu cha waajiri wengi.

Uongozi

Uongozi ni uwezo wa kuwaonyesha njia na kuwahamasisha wengine kufikia malengo mapana ya mwajiri. Kuwa kiongozi maana yake unaweza kujisimamia mwenyewe na kuwasaidia wengine  kuelekea kule kunakotarajiwa na mwajiri.

Uongozi siyo sawa na madaraka. Hizi ni dhana mbili tofauti, lakini zenye uhusiano wa karibu. Unaweza kuwa na madaraka rasmi kazini, lakini katika utendaji usiwe na chembechembe zozote za kiongozi.

Uongozi ni uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa ushirikiano na wengine pasipo kusimamiwa kwa karibu na wakubwa wenye madaraka ya kikazi.

 Uongozi ni pamoja na namna unavyoweza kufanya majukumu mengine kwa moyo wa hiari na kujituma, ili kufikia malengo mapana ya mwajiri. Mtu mwenye tabia za kiuongozi, hahitaji kukasimiwa  madaraka  ili atekeleze wajibu wake.

Uhusiano bora na wengine

Kwa kawaida, kai nyingi zenye tija zinahitaji ushirikano wa karibu wa watu mbalimbali. Ili kuleta ufanisi, kunahitaji uhusiano mzuri wa kikazi baina ya mwajiriwa na watu wengine.

Bila uhusiano mzuri na wengine, pengine kwa sababu ya ile hulka ya kupenda kuwazidi wengine, ufanisi wa pamoja wa kazi husika unaweza kuwa shakani.

Ni kwa namna gani mwajiriwa anaweza kusaidiana na wengine kufanikisha malengo ya mwajiri pasipo ushindani usio na tija? Huu ndiyo  uhusiano unaotakiwa katika kazi.

Mawasiliano

Hakuna uhusiano na wengine pasipo mawasiliano. Mambo mengi katika kazi yanalazimisha wafanyakazi  kufanya mawasiliano yasiyo rasmi kwa kutumia maandishi au mazungumzo ya mdomo.

Kwa mfano, kuna nyakati mwajiriwa atalazimika kuwasilisha taarifa au maoni yake kwa wakubwa wake wa kazi. Pia, atalazimika kuwasiliana na wale anaofanya nao kazi. Hapa ndipo uwezo mzuri wa kuwasiliana unapohitajika.

Ingawa matumizi ya lugha yanatofautiana baina ya mazingira ya kazi,  ni dhahiri katika mazingira mengi ya kikazi, tunalazimika kuelewa namna nzuri ya kuwasiliana na watu. Uwezo wa lugha una nafasi kubwa katika kazi.

Nidhamu ya kazi

Ufanisi katika kazi, kwa kiasi kikubwa, unategemea nidhamu. Namna gani mwajiriwa anaheshimu kazi yake kwa kuwahi kazini, kuwasilisha mrejesho wa kikazi kwa muda hiyo ndiyo inaitwa nidhamu ya kazi.

Aidha, nidhamu ya kazi ni pamoja mpangilio mzuri wa jumla wa majukumu ya kila siku unaotanguliwa na utunzaji wa muda. Mwajiri mzuri hatarajii mtu anayefanya kazi kizembe bila kufuata taratibu za kikazi zilizowekwa.

Uzoefu

Kama  mwajiriwa namna gani unaonyesha ushahidi kwamba una  uwezo wa kufanya kazi inayokusudiwa?  Huo ndio uzoefu. Mwajiri yeyote makini angependa kuona uthibitisho dhahiri kwamba mwombaji wa kazi au mwajiriwa anao uwezo wa kumudu majukumu anayoyaomba kwake au yale aliyoyakabidhiwa.

Uzoefu huu unaweza kupatikana kupita kazi ulizofanya kabla ya ajira husika iwe kwa ajira rasmi au kwa kujitolea. Kwa mtafuta kazi asiye na historia ya kuajiriwa, anahitajika kuutafuta uzoefu kwa  kutafuta fursa za kujitolea za kufanya kazi zinazofanana na ajira anayoitamani, wakati akiendelea na masomo au katika kipindi cha mpito anaposubiri kuajiriwa.

Anza sasa kujiongeza

Ingawa ni kweli kuwa nchi yetu inakabiliwa na ukosefu wa ajira,  ni dhahiri waajiriwa wengi hawaajiriki kwa maana ya kukosa weledi na ujuzi unaowawezesha kuajiriwa na kudumu katika ajira zao.

Ujuzi huu kama tulivyoona, si mara zote unaweza kupatikana kupitia mfumo wa mitihani na vyeti. Ni muhimu kufanya jitihada za makusudi kujinoa kwa lengo la kujiongeza kiujuzi.

Tunapoomba kazi na hata pale tunapotekeleza majukumu yetu kazini, tunawajibika kuthibitisha kuwa ni kweli tunao ujuzi huu mwepesi.

Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Anapatikana kwa [email protected] , 0754 870815.