PIRAMIDI YA AFYA : Vijue vihitarishi vya saratani ya utumbo mpana

Muktasari:

  • Ugonjwa huu hutokana na mambo hatarishi tunayoyafanya katika mienendo na mitindo yetu ya kimaisha ikiwamo matumizi ya tumbaku.

Saratani ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo yameanza kushika kasi katika nchi zenye uchumi ikiwamo Tanzania.

Ugonjwa huu hutokana na mambo hatarishi tunayoyafanya katika mienendo na mitindo yetu ya kimaisha ikiwamo matumizi ya tumbaku.

Kila siku katika mwili wetu kuna mamilioni ya seli zinazoharibika na kufa wakati wa kufanya shughuli mbalimbali za kimwili.Zinapofanya hivyo mwili hujibu mapigo kwa kuzalisha seli za aina hiyohiyo zinazofanya kazi hiyo hiyo kama seli za awali ili kufidia seli zilizokufa. Takwimu za karibuni za nchini Marekani za saratani ya utumbo mpana zinashtua. Marekani kwa sasa inashika namba tatu kwa kusababisha vifo kwa wanaume huku ikishika namba nne kwa kusababisha vifo kwa wanawake

Saratani ya utumbo mpana ni saratani inayojitokeza katika sehemu ya utumbo na eneo la mwisho la utumbo mpana liitwalo puru (sehemu ya kukaa mabaki yasiyohitajika mwilini).

Ukuaji wa saratani hii huanzia katika tando ya ndani ya seli za utumbo mpana baada ya seli hizo kupata mparanganyika na kuanza kujidurufisha kiholela na kusambaa sehemu mbalimbali. Miaka ya hivi karibuni saratani hii hata Tanzania imekuwa ikijitokeza lakini wengi wa wagonjwa hujikuta mara nyingi wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa na hivyo kutotibika na kupoteza maisha. Mojawapo ya dalili za awali pale saratani hii inapopiga hatua ni kama vile kujisaidia damu au choo chenye damu ambacho huwa ni damu nyeusi kidogo, mabadiliko yasiyo ya kawaida ya mfumo wa chakula ikiwamo hali ya kupitisha haja mara kwa mara au kujisikia umetoka haja lakini kama bado haijaisha.

Pia mwili kuwa mchovu muda mwingi na kudhoofika na kupungua uzito kusikoelezeka. Vilevile kuwa na uzito uliokithiri, kutofanya mazoezi, ulaji wa nyama nyekundu kupita kiasi na vitu vilivyokaangwa, kuwahi kupigwa mionzi tiba mwilini. Saratani hii inaweza kuepukwa kwa kupunguza mambo hatarishi, ulaji wa mboga za majani na matunda kwa wingi na kufanya mazoezi mara kwa mara.

Matibabu ya saratani hii inategemea na hatua ya saratani, eneo iliopo, ukubwa wa uvimbe wa saratani na hali ya mgonjwa mwenyewe ilivyo. Unapoona dalili zilitajwa hapo juu ni vema kufika katika huduma za afya kwa uchunguzi wa mapema, kumbuka kinga ni bora kuliko tiba, ugonjwa huu unapopiga hatua za mbeleni unahitaji gharama kubwa sana kuweza kupambana nao.