UCHAMBUZI: Viwanda vya kutengeneza nyaya za umeme visikwamishe umeme vijijini

Hivi karibuni, kaimu meneja wa Shirika la Umeme (Tanesco) mkoa wa Mbeya, Peter Shayo alitoa ripoti ya kazi inayoendelea katika kusambaza umeme wa Rea 111 mkoani hapa.

Katika taarifa yake, Shayo alisema changamoto kubwa katika utekelezaji wa mradi huo ni kukosekana kwa nyaya za umeme baada ya Kiwanda cha East Africa Cable Group kilichoingia mkataba wa kutengeneza na kusambaza nyaya kushindwa kutekeleza kazi hiyo.

Kiwanda hicho kilikuwa kitengeneze nyaya za umeme wa msongo wa kati (MV) na nyingine za msongo mdogo (LV) na kilitakiwa kusambaza tangu Agosti, 2018 lakini hadi sasa hakuna nyaya zilizosambazwa.

Kaimu Meneja katika taarifa yake alisema mkandarasi wa mradi wa Rea 111 ambaye ni Steg International Services ya Tunisia sasa ameamua kuvunja mkataba na kampuni ya East Africa Cable Group baada ya kuona ina udanganyifu.

Hivi sasa mkandarasi ameingia mkataba mpya na kiwanda cha Everwell Cable kilichopo Mkuranga mkoani Pwani ili kitengeneze nyaya hizo.

Hali kadhalika katika taarifa hiyo, Shayo alisema mita za Luku nazo bado hazijafika kutoka China zilikoagizwa, jambo ambalo alisema linaongeza hofu ya mradi kuchelewa kumalizika.

Kwa jumla taarifa hizo ni mbaya kwani zinakwamisha jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ambayo imedhamirisha kusambaza umeme katika vijiji vingi nchini.

Wengi tunaelewa jinsi viongozi wa Wizara ya Nishati wanavyozunguka nchini na kutangaza waziwazi kwamba Serikali imedhamiria kuona vijiji vingi vinakuwa na umeme.

Kutokana na ukweli huo taarifa za kukosekana kwa nyaya na Luku pia kunatakiwa kuwaamsha viongozi mbalimbali wa wizara hiyo ili kutatua changamoto hiyo.

Aidha, kitendo cha kukosekana nyaya hizo kinaweza kuongeza gharama kwa mkandarasi na Serikali jambo ambalo sasa linahitaji kuepukwa.

Kwa upande mwingine, kazi hiyo ikichelewa itasababisha wateja wapya wengi kuchelewa kupata umeme.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shayo, mradi wa Rea 111 mkoani hapa unatarajia kuwafikia wateja wapya 8,387 watakaopatikana katika vijiji vinavyopelekewa umeme kwenye halmashauri za Mbeya vijijini, Rungwe na Busokelo, Kyela, Chunya na Mbarali.

Wananchi wamejipanga kupokea umeme kwa furaha kabla ya mwaka 2020, hivyo ni jukumu la wadau wote wanaohusika kupeleka umeme kutekeleza majukumu yao.

Itakumbukwa kwamba mradi wa kusambaza umeme wa Rea 111 katika vijiji hivyo ulipangwa kutumia muda wa miezi 24 tangu ulipoanza Agosti 2018. Kwa mujibu wa Shayo, mpaka sasa mkandarasi amesimika nguzo kwa asilimia 91.21 ya wigo (Scope) wa nguzo za MV na LV.

Pia hadi kufika Februari 1, 2019, ni vijiji vinne tu ambavyo ni Ilembo, Iyunga Mapinduzi na Madugu vya Mbeya Vijijini na kijiji cha Kifundo kilichopo Wilaya ya Kyela ndivyo vilivyopata umeme wa Rea 111.

Vijiji vingi vikiwamo vya Malamba na Kabale kata ya Suma Rungwe, Kilimansanga kata ya Mpata Busokelo na Mabonde kata ya Msasani Rungwe bado havijaona nyaya za umeme kutokana na kiwanda cha East Africa Cable Group kutotekeleza wajibu wake wa kutengeneza na kusambaza nyaya hizo.

Ni vigumu kuelewa sababu za kiwanda hicho kuingia mkataba wa kutengeneza nyaya ilhali viongozi wake wakijua changamoto zinazokikabili kiwanda chao.

Usumbufu huo unasababisha baadhi ya watu kujenga dhana kwamba wapo walioingia mkataba kwa lengo la kuihujumu au kuikwamisha Serikali kutekeleza malengo ya kupeleka umeme vijijini.

Upo umuhimu wa kufuatilia pia kwa karibu mita za Luku nchini China ambazo zinadaiwa kukwama licha ya kuagizwa siku nyingi.

Hivyo basi Serikali kupitia Wizara ya Nishati haina budi kuingilia kati kwa kuvitaka viwanda vyote vikiwamo vya nguzo na nyaya vilivyopewa kazi ya kutengeneza na kusambaza vifaa vya ujenzi wa miradi ya umeme wa Rea 111 vitekeleze wajibu kuepuka kukwama kwa miradi hiyo.

Hali kadhalika nacho kiwanda cha Everwell Cable hakina budi kujitahidi kutengeneza nyaya bora zinazokidhi viwango kwa lengo la kushika soko ambalo limeachwa wazi na kiwanda cha East Africa Cable Group. Lengo liwe kutekeleza malengo yaliyowekwa.

Lauden Mwambona ni mdau wa maendeleo anayeishi mkoani Mbeya. 0767338897