Vyama vya siasa vijenge mifumo yake imara

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Obama, kwa sasa dunia ina hofu kutokana na watawala wengi kutaka kuongoza kwa ubabe na demokrasia haitiliwi mkazo.

Julai 16, 2018 Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama alitoa hotuba ya kihistoria katika maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

Katika hotuba hiyo aliyoitoa jijini Johannesburg, pamoja na mambo mengine Obama alizungumzia kasumba ya viongozi wengi wa kisiasa barani Afrika kujenga nguvu zao za kisiasa badala ya taasisi imara za uongozi.

Rais huyo mstaafu aliwahimiza viongozi wa bara hilo kujitahidi kujenga mifumo imara ya uongozi ambayo itasaidia maendeleo barani Afrika hata pale watakapoondoka madarakani.

Obama aliwataka viongozi wa kisiasa kuacha kufikiria kujijenga wao zaidi katika uongozi badala yake wafikirie kuzijenga taasisi zao kuwa imara kwa faida ya wananchi.

Kwa mujibu wa Obama, kwa sasa dunia ina hofu kutokana na watawala wengi kutaka kuongoza kwa ubabe na demokrasia haitiliwi mkazo.

Nitajadili kwa ufupi mgogoro uliokuwapo wa kisiasa ndani ya Chama cha Wananchi (CUF).

Migogoro mingi katika vyama vya siasa na taasisi nyingine inatokana na viongozi kutojenga mifumo imara ya uongozi katika vyama au taasisi zao, na badala yake watu hujijenga zaidi ili kuogopwa na wengine kama vile wataishi milele.

Faida za kiongozi kuwa na nguvu zaidi ya taasisi hazidumu kwa muda mrefu kwani, lazima kuna wakati kiongozi atalazimika kuwateua wengine kwa kupenda au kutopenda, lakini taasisi itaendelea kuwepo.

Kinachotokea leo katika mgogoro ndani ya CUF hakina tofauti sana na wosia wa Obama kwa viongozi wa kisiasa barani Afrika kuacha kujenga nguvu zao katika vyama, bali wajenge mifumo imara yenye nguvu.

Kabla ya kuondoka kwa Maalim Seif kilichokuwa kinaendelea katika chama hicho ni wazi kinagusa ushauri wa Obama kuwa, taasisi au vyama vinapokuwa dhaifu katika uongozi na kuruhusu viongozi kuwa na nguvu zaidi mwisho wake ni vurugu.

Mgogoro kama huo umeviua vyama vingi barani Afrika vikiwamo hata vile ambavyo vilishiriki kuleta uhuru kwa baadhi ya mataifa kwani nguvu za viongozi zilivigawa na mwisho kupotea katika historia.

Funzo kubwa la vyama vya ukombozi kutoweka kutokana na migogoro ya nguvu za viongozi wao ni nchini Kenya ambako kulikuwa na Chama cha Kanu kilichoongozwa na Jomo Kenyatta, lakini leo hii imebaki historia.

Nchini Zambia kulikuwa na Unip iliyoongozwa na Kenneth Kaunda, leo pia nguvu yake imebaki historia katika medani za kisiasa na pia kule Malawi tunakikumbuka chama cha Malawi Congress cha Kamuzu Banda, lakini leo hii hakina nguvu tena. Historia ya kutoweka kwa vyama vikubwa vya kisiasa barani Afrika ni ndefu na inapaswa kuwa funzo hapa nchini kwa viongozi wetu kutambua dhamana wanayopewa kuwa wanapaswa kuitumia vizuri kuimarisha vyama vyao na siyo kujiimarisha wao.

Miongoni mwa sababu kubwa ambazo zinaviangusha vyama hivi ni viongozi kujali masilahi yao binafsi na kuondoka katika misingi ya kuanzishwa kwa vyama vyao.

Kwa kawaida vyama vina katiba zake, lakini ni aghalabu kufuatwa badala yake matamko na matakwa ya viongozi wa vyama ndiyo yamekuwa mwongozo jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wake.

Leo hii kinachotokea CUF ni pigo kubwa kwa upinzani nchini kwani athari zake hazitaishia katika chama hicho pekee, bali itavitafuna vyama vingine ambavyo viongozi wake wamekuwa hawafuati katiba za vyama vyao.

Ingawa mgogoro wa CUF umeamuliwa mahakamani, lakini suluhu yake ni ngumu kupatikana hasa kutokana na chama hicho kujengwa na nguvu za viongozi wake kuliko mifumo imara ya kiuongozi.

Ni wazi kuwa mdudu ambaye leo anaitafuna CUF ndiye huyohuyo ambaye amepunguza nguvu ya vyama vingine kama NCCR - Mageuzi, UDP na TLP.

Itoshe kukumbushia kauli ya Obama kuwa, ni muhimu viongozi wa kisiasa na taasisi nyingine wakajitahidi kujenga mifumo imara ya kiuongozi katika taasisi zao badala nguvu za viongozi.

Pia, ili kuwa na taasisi imara, ni vyema katiba kufanyiwa maboresho ya mara kwa mara kuondoa mazingira ya kuwapa nguvu kubwa viongozi badala ya vyama.

Naamini tukiendelea na mifumo yetu ambayo inawajenga viongozi kuwa na mabavu ya kufanya walitakalo bila kufuata katiba za vyama tutegemee vyama kuingia katika migogoro isiyokwisha.

Mussa Juma ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Arusha