UCHAMBUZI: Vyama vya ushirika vilete mapinduzi ya kilimo

Friday August 9 2019

Chama cha ushirika huanzishwa na watu wenye jambo linalowaunganisha. Kwa wakulima maskini wanaolima na kufuga, chama hicho huwaunganisha ikiwa ni njia ya kujikwamua dhidi ya matatizo ya kiuchumi. Bila chama cha ushirika, mkulima na mfugaji hufuga na kulima kwa mazoea, hasa kuhamahama.

Mkulima analima mazao bila kutumia njia bora za kilimo. Anatumia jembe, shoka na panga kufyeka msitu na kuchoma mabiwi, kisha shamba linakuwa limepatikana. Anapanda mbegu bila kuweka mbolea ili tu azalishe mali kukidhi mahitaji yake na familia, kisha ziada ya kuuza sokoni inakuwa haipo.

Kama ikiwapo, basi inakuwa ni ndogo isiyomuweza kuboresha maisha yake na familia. Kwa kawaida wakulima hufuga na kulima mazao mbalimbali ya chakula na biashara. Mazao hayo yapo ya muda mfupi na muda mrefu.

Mazao hayo hulimwa nchini kufuatana na hali ya hewa na aina za udongo, hivyo wakulima wadogo wakianzisha vyama vya msingi vyenye madhumuni mengi, watazalisha mifugo bora na mazao ya kilimo yenye tija kwa kuwa wanatumia pembejeo za zama bora za kilimo.

Pia, wataalamu wa ushirika na kilimo ni rahisi kuwapa elimu ya kukuza ushirika na kilimo chao.

Vyama hivi ni mkombozi vijijini badala ya kulima zao moja la biashara, wanalima mazao zaidi ya moja na kufuga. Mkazo wa kulima zao moja kama katani, kahawa, karafuu na kuachana na mazao mengine ni tatizo katika bei ya soko la dunia.

Advertisement

Bei ikishuka mkulima hupata hasara na pia pato la Taifa hupungua, hivyo mipango huvurugika na kutopata pato la kutosha kugharamia mipango mingine ya maendeleo nchini. Hii ina maana kuwa ni vyema kuachana na mazao ya biashara tu, bali kulima na mazao mengine pia ili mkulima awe na pato la uhakika wakati wote.

Katika uchumi upo usemi usemao: “Weka mayai ya viwandani katika vikapu tofauti.” Maana yake ni kwamba mtu awekeze katika uzalishaji wa mali mbalimbali kama kinga ya hasara katika eneo moja linaloweza kutopata faida lakini katika eneo lingine ukapata, hivyo maisha kuzidi kuboreka.

Sera ya vyama vya ushirika ni vyema ishirikishe viongozi na wataalamu mbalimbali kwa kufahamu kwamba nchi yetu ina makabila mbalimbali yenye mila, desturi na mitazamo tofauti ya maisha.

Wako wakulima wadogo wanaolima na kufuga katika maeneo yanayofahamika, wapo wafugaji wanaohama hama na mifugo kutafuta malisho.

Pia, lipo kundi la watu linarandaranda misituni kuwinda wanyama kwa ajili ya chakula. Viongozi wa vijiji watumie wataalamu wakiwamo wanasosiolojia na wanasaikolojia, hasa walimu wa elimu ya watu wazima katika mipango yao ya maendeleo ya kilimo, uchumi, ushirika, ardhi, misitu na maji.

Wanasiasa katika maeneo yao wahamasishe wananchi ili wabadilike na kuwafanya wahamie kwenye makazi yao kudumu badala ya kuhama hama.

Pia, wanaushirika wazingatie mambo yafuatayo; kwanza wawe na lengo la kukuza kilimo na ufugaji bora, pamoja na kupanda miti. Pili , wachague eneo linalofaa kwa kilimo na ufugaji ambalo halina mgogoro. Eneo la wakulima liwe limepimwa na kuwekwa mawe.

Tatu, watu wanaorandaranda maporini kutafuta wanyama wawe na eneo lililowekewa mawe. Na kila familia iwe na eneo la ardhi sio chini ya eka 10 na muda wa kumiliki ardhi uwe wa kipindi kirefu. Pia, wakulima wawezeshwe matrekta kwa ajili ya kilimo.

Mfuko wa pembejeo unaweza kuwezesha watu zana za kilimo. Pia, kampuni mbalimbali zishawishiwe kuwekeza ili kukuza kilimo na ufugaji.

Haki miliki ya ardhi kwa mkulima au mfugaji ni hakikisho kwa wawekezaji kuhusu usalama wa mali zao.

Hata hivyo, kundi la wafugaji halina tatizo la mtaji kwa kuwa wanayo mifugo mingi ya ng’ombe wanaoweza kusababisha wawe na fedha za kugharamia kilimo na ufugaji bora katika makazi yao.

Wataalamu wa ushirika, kilimo, maji, mifugo, ardhi na misitu wahamasishe watu umuhimu wa kilimo bora kabla ya kuhamia katika makazi mengine. Elimu iwe ya matumizi bora ya ardhi na upandaji miti. Mrajisi wa vyama vya ushirika, awasomee maofisa ushirika na kuwafafanulia kuhusu sheria na kanuni za ushirika ili waboreshe pale inapohitajika.

Pia, chama kiwe chenye ukomo wa madeni maana yake ni kwamba chama kiuze mali za ushirika kulipa madeni ili wanachama wawe salama kwa kutouzwa mali zao kama nyumba na vitu vingine.

Maofisa ushirika wapitishe makisio ya vyama hivyo kabla ya kupelekwa kwa taasisi za kifedha ili kuomba mikopo ya kununua mazao, pembejeo za kilimo na kujenga maghala. Njama Mnondwa ni msomaji wa gazeti hili anapatikana kwa namba 0784603570 Handeni, Tanga.