UCHAMBUZI: Vyama vya ushirikia vikiwatambua vijana, kilimo kitaimarika

Mara kadhaa, husemwa kuwa vijana ni jeshi kubwa la jamii ingawa ushawishi wao kiuchumi ni mdogo.

Mambo kadhaa yanahitaji kufanywa ili kuwapa nafasi ya kuchangia kukuza uchumi wa Taifa hivyo kupunguza umasikini uliotamalaki nchini.

Miongoni mwa maeneo hayo ni kuwajumuisha kwenye vyama vya ushirika ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa na mchango mkubwa wa kuwainua wakulima wa mazao tofauti kabla ya hivi karibuni havijaonyesha umuhimu wake kwa makundi maalumu hasa wanawake.

Historia ya ushirika Tanzania inatokana na uhitaji wa kutatua changamoto za masoko ya mazao ya wakulima wadogo waliokuwa hawapati soko la uhakika la mavuno yao.

Tanzania inafahamika duniani kwa kilimo cha mazao tofauti ya biashara ambayo, hata hivyo hayawashirikishi vijana. Wakulima wengi ni wanawake.

Kutokana na kusahaulika kwa vijana, kilimo hakikui kwa kasi kubwa kuweza kundoa umasikini uliopo nchini. Hali hiyo inatokea ingawa kuna idadi kubwa ya mazao ya biashara ambayo yangeweza kuwaajiri vijana wengi wanaorandaranda mtaani.

Hali iko hivyo licha ya mazao hayo ya biashara ambayo ni pamoja kahawa, pamba na korosho kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa. Kahawa ndilo zao lililojaa historia kubwa ya ushirika hasa Tanzania kwenye mikoa ya Kilimanjaro na Kagera.

Ingawa hivi sasa ushirika unahamasishwa kwenye mazao mengine mfano korosho zinazolimwa zaidi mikoa ya Kusini inayojumuisha Mtwara, Lindi na Ruvuma, lakini kahawa ndio inayobeba historia ya ushirika nchini.

Mazao haya yana asili ya kuishi na kustawi kwa muda mrefu hata biashara yake haina mzunguko wa haraka hivyo kuhitaji uvumilivu. Kwa kiasi kikubwa, mazao haya ni uwekezaji wa watu wenye umri mkubwa na wamedumu kwenye mazao haya na ushirika wa kilimo na masoko aina hii kwa miongo kadhaa sasa wakipambana na changamoto nyingi.

Kwa miaka 10 hivi nyuma, vijana wengi wameingia kwenye kilimo cha matunda na mbogamboga ambayo hulimwa kisasa na kustawi baada ya muda mfupi. Mazao haya yanajumuisha vitunguu, karoti, pilipilihoho, mboga za majani, matunda kama vile matikitimaji, matango, maparachichi, maembe, nanasi na mengine. Hiki ni kilimo ambacho kinawavutia vijana wengi hivyo kuhitaji mikakati endelevu.

Changamoto za mtaji, pembejeo na nyinginezo nyingi zinaweza kujibiwa kwa kuipa nafasi sekta ya ushirika kuingia kwenye kilimo biashara hiki.

Faida za kuwa kwenye vikundi vya ushirika ni kupatikana kwa mtaji nafuu wa kuanzia na kupanulia kilimo.

Faida nyingine ni kutatua changamoto za masoko na bei. Ifahamike kwamba, pamoja na mwenendo mzuri wa kilimo hiki bado changamoto za masoko na bei za bidhaa hizi, wakati wote, hazilingani na gharama za uendeshaji hivyo ni muhimu kuwa na nguvu ya pamoja ya ushirika kutafuta masoko na kuweka mikakati ya bei nzuri itakayowanufaisha wakulima ambayo haitawaumiza walaji pia.

Mafunzo ya matumizi ya teknolojia mpya za kilimo kwa bei ya chini ni majukumu mengine yanayoweza kutekelezwa na chama cha ushirika kinachoweza kutafuta fursa hizo na kurahisisha upatikanaji wa mbegu, mbolea na vifaa vya umwagiliaji jambo litakalowanufaisha wanachama wake tofauti na mtu akiwa peke yake.

Kufanikisha haya tunahitaji kwanza kufuta dhana ya ushirika kuwa ni kitu kibaya. Watu wabuni mbinu mpya za kufanya sekta hii kuwa ya kuwafaidisha wengi. Ni muhimu kwa vyama vitakavyoanzishwa kutokana na kilimo cha matunda na mbogamboga kuangalia uwezekano wa kupunguza maeneo ya kudhoofisha ufanisi na ubora wa chama kwa kuweka mifumo mizuri na ya kisasa ya kutunza taarifa za fedha na ufanyaji utendaji wa chama chao.

Kuwajibika vizuri kwa wajumbe wa bodi wenye weledi na maono mazuri na kushiriki vyema kwenye shughuli za chama kwa kuhoji, kushauri na kutumia huduma vizuri.

Kuwapo ubunifu wa miradi, miongozo na ushawishi ili kuwasogeza vijana na wakulima wa mazao ya kibiashara kuingia kwenye vikundi na vyama vya ushirika ili kupiga hatua kwenye uzalishaji na masoko ya uhakika.

Itapendeza sana tutakapokuwa na vyama vipya vinavyoundwa na wakulima wa matunda na mbogamboga. Itakuwa faraja kwa sababu itaurudisha ushirika mikononi mwa vijana wengi waliojiingiza kwenye kilimo kinachokwenda na kasi ya mabadiliko ya sayansi za uzalishaji na masoko. Mamlaka husika zisaidie kuhakikisha mambo haya yanafanikiwa.

Mwandishi ni mtaalamu wa masuala ya ushirika. Anapatikana kwa namba 0657 157 122.