Waathirika wa ukatili sasa kupata huduma za kisheria, tiba hospitali

Wakati mwingine jeraha lililotokana na kupigwa au kubakwa linaweza kumsababishia mwathirika athari zaidi hasa kifo endapo atachelewa kupatiwa huduma.

Hilo hutokea kama atakuwa amepoteza damu nyingi kwa kipigo na anaishi mbali na kituo cha polisi anachotakiwa akachukue fomu namba 3 (PF3) kwa ajili ya kupata matibabu.

Kutokana na kuongezeka matukio ya ukatili wa kijinsia nchini, takribani vituo 12 vinajulikana kama One Stop Centre (OSC), vimejengwa katika baadhi ya hospitali ili kuwaondolea usumbufu waathirika wa matukio hayo.

Hospitali ya Mwananyamala pekee mwaka 2016 ilipokea taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia 108 na mwaka jana yaliongezeka hadi kufikia 350.

Februari mwaka huu hospitali hiyo ilikabidhiwa kituo hicho kilichojengwa na Shirika la Utu wa Mtoto chini ya Ufadhili wa Shiri-ka la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu Duniani (UNFPA).

Kuanzishwa kwa kituo hicho, jamii itapata huduma za ustawi wa jamii, matibabu, polisi na watu wa sheria kwa kuwa wote wanatoa huduma kwa pamoja.

Lengo la vituo hivyo kujengwa katika vituo vya afya ni kuhakikisha huduma za matibabu zinatolewa haraka.

Ofisa utumishi wa utawala wa hospitali hiyo, Mansour Karama anasema kutokana na kuwapo kwa kituo hicho, matukio yatokanayo na ukatili wa kijinsia yatashughulikiwa ipasavyo.

“Mwaka 2017 tulipokea matukio 219; kati ya hayo 164 yalihusu wanawake na 55 wanaume,” anasema Karama.

Pia, anasema asilimia 79 ya matukio hayo ilikuwa inahusu ukatili wa kingono.

Katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Dk John Jingu anasema kuwapo kwa kituo hicho kutawezesha usalama wa waathirika kwa kupata huduma kamili ikiwamo za afya na sheria.

“Awali, mtu alikuwa akifanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwamo kubakwa au kulawitiwa analazimika kwenda kwanza kituo cha polisi ili apate fomu ya polisi namba tatu maarufu PF3, ndiyo aende hospitali kupata matibabu.

“Muda unakuwa umepotea hapo, bado hajapata huduma ya kisheria na ushauri nasaha hivyo ilikuwa ngumu kufikia huduma hizo zote.

“Tumemsikia Karama (ofisa utumishi Hospitali ya Mwananyamala) akitoa takwimu zikionyesha matukio yanayohusiana na ukatili wa kijinsia yanaongezeka; pengine kungekuwapo na mazingira mazuri, salama na ya faragha taarifa za matukio hayo zin-geongezeka zaidi,” anasema Dk Jingu.

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Koshuma Mtengeti anasema kituo hicho kitawasaidia kupata taarifa za kesi mbalimbali za ukatili wa kijinsia zilizolipotiwa kituoni hapo kwa ajili ya mipango ya baadaye katika kuboresha kazi zao.

Mtengeti anasema kituo hicho kitasaidia kuimarisha uwezo wa watoa huduma ili kufikia dhima ya mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Anasema pia, kitatoa huduma bila gharama kwa mtu atakayethibitika amefanyiwa ukatili.

“Lengo ni kuwawezesha waathirika wa ukatili wa kijinsia kupata huduma kamili za kiafya, kisaikolojia, usaidizi wa kisheria, ushauri nasaha na huduma za polisi ikiwa ni pamoja na utoaji wa PF3; pamoja na kuhakikisha haki na usalama kwa waathirika unazingatiwa,” anasema Mtengeti.

Ukatili wa kingono

Akizungumzia ukatili anasema upo wa aina nyingi dhidi ya wanawake na watoto ukiwamo wa kingono na kimwili.

Mtengeti anasema takwimu za Serikali zinaonyesha kuwa katika kila watoto watatu wa kike, mmoja amefanyiwa ukatili wa kingono.

Pia, anasema katika kila wasichana 100, kati yao 37 wanaolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18, kuhusu mimba za utoto mwaka 2010 zilikuwa asilimia 23 huku mwaka 2015 ilifikia asilimia 26.

Mtengeti anasema kutokana na hali ya matukio ya ukatili wa kijinsia yanayoendelea, changamoto ni upelelezi unaokwamishwa na wananchi kwa kutotoa ushirikiano na ushahidi wa kutosha kwa polisi.

Mkuu wa utawala na rasilimali watu na vifaa; ACP Debora Magiligimba anasema vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vimekuwa vikiongezeka huku takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha Januari na Oktoba 2018, kesi za kubaka zilizoripotiwa jijini Dar es Salaam ni 714.