Wagonjwa wanaowekewa betri za moyo waongezeka

Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imesema idadi ya wagonjwa wanaohitaji kuwekewa vifaa vinavyosaidia kurekebisha mapigo ya moyo ‘Pacemaker’ wanaongezeka nchini.

Ilielezwa kuwa ikilinganishwa na awali, hivi sasa wanaohitaji huduma hiyo wanafikia 40 kwa mwezi kutoka watatu.

Akizungumza mapema wiki hii na jarida hili, Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya moyo kutoka taasisi hiyo, Peter Kisenge alisema ongezeko hilo limetokana na elimu inayotolewa mara kwa mara.

“Wanaofika kupokea matibabu hapa idadi yao imeongezeka watu wameanza kupata uelewa kwamba tunafanya nini kwa mfano hivi sasa tunaweka betri za moyo kwa mwezi tunaweza kuwawekea wagonjwa 20-30 wanaohitaji upandikizwaji wa betri hizo hapo awali tuliweka kwa wagonjwa watatu mpaka wanne,” alisema Dk Kisenge.

“Tunapandikiza mishipa ambayo imeharibika na kutibu magonjwa mengine hivyo tuwaombe madaktari popote walipo waitumie hii taasisi kuleta wagonjwa ili wananchi wafaidike na huduma,” alisema.

Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Profesa Mohammed Janabi alisema taasisi inazidi kuimarika kadri miaka inavyokwenda.

“Tunafanya oparesheni ngumu zaidi kadri siku zinavyokwenda, mgonjwa mdogo kabisa kwa sasa mtoto wa wiki mbili na mkubwa ni wa miaka 82 tunaamini miaka mitano kutoka leo tutaanza kufikiria kupandikiza moyo au kufanya nini ili kuja na matibabu ya juu zaidi,” alisema Profesa Janabi.

Alisema kwa kipindi cha mwaka 2018 pekee, JKCI ndiyo taasisi ya moyo iliyofanya upasuaji mwingi katika nchi za Afrika ukiachilia Afrika Kusini ambayo iliongoza.