UCHAMBUZI: Wakazi visiwa vya Kanda ya Ziwa wapewe elimu ya afya

Friday August 9 2019Jonathan  Musa

Jonathan  Musa 

Mtu kuwa na maarifa au uelewa wa jambo fulani huwa na faida tofauti na asiye navyo.

Kwa mfano, mzazi asiyefahamu maana ya elimu, hawezi kuwa na nia wala kutilia mkazo jambo hilo kwa watoto wake. Haoni wala hajui umuhimu wake.

Mzazi wa aina hiyo lazima atakuwa na vikwazo tena aghalabu huku akionyesha mifano kwamba mbona fulani hajasoma lakini ana mafanikio!

Kwa mfano, katika Kijiji cha Bwisya, Kata ya Ukara wilayani Ukerewe, nilishuhudia makubwa baada ya Kivuko cha MV Nyerere kuzama Septemba 20, 2018 na kuangamiza zaidi ya watu 200.

Katika kipindi hicho cha hekaheka, shughuli nyingine zilikuwa zikiendelea katika eneo hilo la ziwani.

Licha ya mafuta mengi kumwagika ziwani pamoja na kuwapo miili ya watu waliozama, wananchi wa maeneo hayo walikuwa wakiendelea na matumizi ya maji hayo kama kawaida.

Advertisement

Mwanzoni nilidhani maji waliyokuwa wakichota yalikuwa kwa ajili ya kumwagilia sakafu au majengo, lakini nilikuja kubaini kwamba baadhi yao walichota maji hayo mita chache kutoka kilipokuwa kivuko cha MV Nyerere na kupeleka nyumbani kwa ajili ya matumizi, yakiwamo mapishi na kunywa.

Maji haya yalikuwa na mafuta aina ya dizeli, grisi achilia mbali uchafu mwingine. Hii ina maana kwamba waliokuwa wanayatumia walikunywa kemikali zitokanazo na mafuta hayo na aina nyingine ya taka na masalia yaliyokuwa kwenye meli.

Kwa hili nililoshuhudia, ni wazi kuwa elimu inatakiwa kutolewa kwa wananchi hawa. Huenda hawaelewi madhara ya kunywa maji yaliyokuwa na chembechembe za mafuta ya dizeli.

Mbali ya hilo, nilibaini kuwa elimu hiyo ni muhimu zaidi kwani katika Kata ya Ukara, kuna visiwa ambavyo vina nyumba chache lakini idadi ya watu ni kubwa na kibaya zaidi nyumba hizo hazina sehemu maalumu za kujisaidia. Nilidokezwa kuwa baadhi humaliza haja zao ziwani.

Lakini, mwenyekiti wa Kijiji cha Bwisya, Oru Mageru anasema uelewa mdogo na ukosefu wa maarifa miongoni mwa wananchi ndio chanzo cha wao kukumbwa na homa ya matumbo na amoeba.

Anasema mara kwa mara wamekuwa wakitoa elimu kuhusu madhara ya kutumia ovyo maji ya ziwani akibainisha kuwa baadhi ya kaya hujisaidia humo.

Mbali na kisiwa hicho, hali ni hiyohiyo katika mwalo wa Ibanda, Kata ya Kirumba wilayani Ilemela. Wananchi wengi wameshudiwa wakifua na kuosha vyombo vya jikoni ziwani.

Sidhani kama jambo hilo ni sahihi ikizingatiwa kwamba ziwa hilo limejaa masalia ya aina mbalimbali kama vile mizoga na uchafu mwingine ambao unaweza kuwa sumu zinazotumiwa bila tahadhari na wananchi.

Hali hiyo inawaweka wananchi hao katika hatari kubwa, kama kupata maradhi yanayoweza kugharimu nguvu kazi ya taifa lakini pia gharama kubwa kuyatibu.

Siku chache zilizopita, mama mmoja aliripotiwa kushambuliwa na mamba.Mwanamke huyo aliyefahamika kama Grace kutoka Wilaya ya Sengerema, alivamiwa na mamba huyo baada ya kumaliza kufanya usafi wa vyombo vya jikoni na nguo katika ziwa.

Wakazi wengi wa visiwani na wale waishio kandokando mwa mialo, wamekuwa na mazoea ya kutumia maji haya kwa njia ya mkato ili kujirahisishia majukumu.

Hilo linawaweka katika hatari kubwa kiafya pamoja na mashambulizi kutoka mamba na viboko kama ilivyokuwa kwa mama huyo.

Kiongozi mmoja wilayani Ukerewe anasema asilimia kubwa ya watu visiwani hawajazoea matumizi ya maji.

Ofisa afya mmoja wa afya ambaye ni mstaafu anasema wananchi wengi kisiwani hapo hawapendi kufundishwa na mara nyingi imani zao zimekuwa kikwazo katika kubadili mitazamo yao.

Hii imechangia kwa kiwango kikubwa wananchi hao kufikwa na maradhi ya tumbo na kuvamiwa mara kwa mara wa mamba.

Licha ya madhara hayo kuonekana wazi, somo la kubalika limekuwa gumu miongoni mwa wengi wao.

Kaya nyingi wilayani Ukerewe na Kanda ya Ziwa hasa za visiwani na kandokando mwa ziwa, hazina uelewa wa kutosha wa kinachoweza kutokea baada ya kuchafua mazingira au kutumia maji machafu.

Huenda elimu ikitolewa, wananchi watabadilisha mitazamo yao na kesi za kulazwa hospitalini kwa kuumwa tumbo zitapungua.

Jonathan Musa ni mwandishi wa gazeti hili anapatikana kwa simu namba 0744 205 617