Wakurugenzi mmemsikia Waziri Ummy Mwalimu kuhusu mikopo?

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Muktasari:

  • Akizungumza katika sherehe hizo zilizohusisha wanawake wa wilaya za Misungwi, Nyamagana, Ilemela na Magu, Waziri Ummy alisema hatamvumilia mkurugenzi anayetoa mkopo usiokuwa na tija kwa wanawake.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewaonya wakurugenzi wa halmashauri za miji na majiji kuacha tabia za kuwapatia mikopo wanawake isiyokuwa na tija.

Kwa mujibu wa waziri Ummy, ataanza kuwachukulia hatua wale wote watakaokiuka maelekezo yaliyotolewa na Serikali.

Kauli ya Ummy ilitolewa mwishoni mwa wiki kwenye sherehe za kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Machi 8, mwaka huu zilizofanyika kwenye viwanja vya Bunjora wilayani Magu wakati alipokuwa akihutubia.

Waziri Ummy alisema Serikali imepitisha sheria kwa kila halmashauri kutenga asilimia nne kutoka kwenye pato la ndani kwa ajili ya mikopo ya akina mama wanaojishugulisha na ujasiriamali.

Alisema tangu sheria hiyo ipitishwe mwaka 2016/17 kiasi cha Sh8.3 bilioni zilitolewa na 2017/18 zilitengwa jumla ya Sh16 bilioni ambazo ni mikopo kwa ajili ya wanawake.

Alisema Serikali itaendelea kuboresha zaidi utoaji wa mkopo huo wenye riba nafuu huku akiagiza kila halmashauri kuorodhesha kiasi cha fedha kilichotolewa kutoka mwaka 2016 pamoja na idadi ya waliopokea mikopo hiyo.

Akizungumza katika sherehe hizo zilizohusisha wanawake wa wilaya za Misungwi, Nyamagana, Ilemela na Magu, Waziri Ummy alisema hatamvumilia mkurugenzi anayetoa mkopo usiokuwa na tija kwa wanawake.

Ummy anasema kumekuwapo na tabia za baadhi ya wakurugenzi kuwapatia kiasi cha Sh500, 000 hadi 1,000, 000 kikundi cha watu 25 hadi 30 kiasi ambacho wakigawana hakikidhi matakwa yao.

Waziri huyo alisema fedha wanazopatiwa wajasiriamali hao hazitoshelezi kuanzisha biashara yoyote badala yake wanawapa za matumizi yao wenyewe.

Alisema ataanza kupita kwenye kila halmashauri kukagua maendeleo ya fedha hizo kwani wapo wakurugenzi wasiotekeleza maelekezo hayo.

Aliwataka pia maofisa maendeleo kuhakikisha wanafuatilia kwa kina vikundi vinavyowezeshwa kujua maendeleo yake halikadhalika kuvipatia ushauri.

Kauli ya waziri huyo imekuja huku kukiwapo malalamiko mengi ya vikundi vya akina mama wakidai mikopo hiyo haina tija kwao kwa kuwa haiwasaidii kuendeleza biashara zao.

Akizungumzia suala hilo mmoja wa wajasiriamali mkazi wa Mabatini jijini Mwanza, Asha Maulid alisema mkopo wanaopatiwa ni mdogo huku pia muda wa marejesho ukiwa ni mfupi.

Asha anadai kuwa kulingana na hali ya uchumi ilivyo kwa sasa wanashindwa kuzalisha hivyo kuingia katika hasara kubwa.

Ni wakati sasa kwa wakurugenzi kujitafakari na kuanza kutoa mikopo yenye tija lengo ikiwa ni kuwakwamua na umaskini wanawake kama ilivyokusdiwa.

Naipongeza Serikali kwa kutengeneza mazingira ya usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu, lakini ombi langu kwa wakurugenzi na maofisa maendeleo wajikite kuwapatia elimu ya ujasiriamali ili waweze kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa kwani wapo wanawake ambao badala ya kutumia fedha hizo kwa kuanzisha biashara au kilimo huzitumia kwa mambo mengine yasiyokuwa na tija hali inayosababisha kuingia hasara.

Naamini kutokana na mazingira yaliyopo sasa mwanamke hatakiwi kufanya kazi kwa ajili ya kupata fedha ya chakula kwa siku hiyo tu badala yake kujijengea uhuru wa kiuchumi.

Ni vyema mikopo inayotolewa na halmashauri kwa makundi maalumu ikawanufaisha zaidi na kuitumia katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na shughuli za kilimo, ufugaji au biashara nyingine ili kusaidia katika mapambano dhidi ya umasikini.

Pia, mafanikio hayawezi kufikiwa endapo jamii haitakemea vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake kwa kuwa vinarudisha nyuma juhudi za maendeleo.

Tayari Serikali imeunda Mpango wa Kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake (Mtakuwa), ambao utaenda sambamba na kutokomeza mimba za utotoni kwa zaidi ya asilimia 20 ifikapo mwaka 2021.

Hivyo, kupitia mpango huo Serikali inashauri kila mtaa iunde kamati za ulinzi wa mtoto na mwanamke lengo ni kuhakikisha tunatimiza malengo.

Ni imani yangu vita dhdi ya ukatili itaenda sambamba na kumuwezesha mwanamke kuweza kusimama kwa kuinua kipato chake ili aweze si kuihudumia familia yake bali kuchochea uchumi wa Taifa.

Kwa maoni na ushauri; [email protected]