UCHAMBUZI: Walemavu wana haki sawa kama Watanzania wengine

Wednesday November 13 2019Sada Amir

Sada Amir 

By Sada Amir

Katika watu wanaotaabika kwenye suala zima la mawasiliano , ni watu wenye ulemavu hasa wasioona na wenye ulemavu wa kusikia.

Ukiachana na mawasiliano ya kawaida kati ya watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu, kundi hilo linapata changamoto sana kwenye suala zima la mawasiliano kwa njia ya simu.

Wakiwa kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mawasiliano na Baraza la Ushauri la Watumiaji Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA CCC), mkoani Mwanza wiki iliyopita kilicholenga kuboresha sekta ya mawasiliano kwa kukusanya maoni kutoka kwa watu wenye ulemavu; walisema changamoto kubwa wanazokutana nazo ni wao kuwekwa kando na kusahaulika linapokuja suala zima la elimu ya watumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano.

Aidha, walisema miundombinu inayotumika kutoa elimu ya huduma na bidhaa za mawasiliano si rafiki wakitolea mfano vipeperushi vinavyotolea huduma havina alama ya nukta nundu ambayo hata mtu asiyeona anaweza kusoma mwenyewe na kuelewa vizuri.

Kwa upande wa viziwi wanapata shida wanapoenda kwenye ofisi za makampuni ya huduma za simu kupata huduma mbalimbali ambapo wakifika kwenye ofisi hizo huishia kutoelewana kwa sababu ya ‘lugha gongana’ kati ya watoa huduma kwa wateja na wateja wenyewe ambao ni viziwi.

Lugha inagongana kwa sababu hakuna wakalimani kwenye ofisi hizo ambao ni muhimi na ni haki kwa wateja wenye matatizo ya kusikia hivyo wateja hao wanaondoka bila kupata huduma waliyoikusudia.

Advertisement

Katika ofisi zinazohudumia umma, wakalimani wa lugha za alama ni muhimu sana kwa sababu ofisi hizo si tu zitahudumia watu wanaosikia vizuri bali hata wasiosikia, hivyo ni jukumu la makampuni ya huduma za simu kuweka watu wanaoweza kuzungumza lugha za alama kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa kusikia na wa kuongea.

Ofisa elimu na uhamasishaji Baraza la Ushauri la watumiaji wa huduma za Mawasiliano nchini (TCRA Ccc), Hirali Tesha aliahidi kuwa watakaa na Serikali na wadau wengine wa mawasiliano ikiwamo TCRA na watoa huduma kuona namna gani wanahakikisha na walemavu ambao ni sehemu ya watumiaji wa huduma za mawasiliano wanapata haki yao ya msingi.

Iwapo hilo litatokea, litawawezesha wenye ulemavu huo kuwasiliana na kupata huduma bila ya changamoto wanazopitia kwa sasa.

Hatua hiyo itaiwezesha jamii iwe mstari wa mbele kushirikiana na watu hao kwa kutowanyanyapaa hasa pale wanapohitaji msaada.

Kwa vile uelewa wa kundi hili pia ni mdogo juu ya suala zima la huduma za mawasiliano, wadau mbalimbali wakiwamo mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na TCRA yenyewe waongeze uwezeshaji kwa kundi hilo ili lipate taarifa mbalimbali na waongeze miundombinu rafiki na vipeperushi vyenye alama ya nukta nundu kwa ajili ya watu wasioona.

Huduma zinazoweza kuwafaa watu wasioona ziwepo, kwa mfano jarida la mwongozo kwa watumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano la mwaka 2019 lililotolewa na TCRA lingekuwa na alama za nukta nundu walemavu wa macho wangefaidi.

Majarida hayo yana mambo muhimu yaliyokusudiwa kumwezesha mtumiaji wa huduma za mawasiliano kujilinda dhidi ya matukio mbalimbali, kusababisha athari zikiwamo za upotevu wa mali.

Kwa kuzingatia haki za watumiaji wa mawasiliano ambazo ni kupata huduma bora, kupewa taarifa kuhusu huduma na bidhaa, baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za mawasiliano lina jukumu la kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata huduma stahiki na bora.

Lakini na watumiaji wa mawasiliano ni jukumu lao kutimiza wajibu wao hasa wajibu wa kuhakikisha wanapata elimu inayohusu mada husika hata kama ni kwa kuwasiliana na wahusika moja kwa moja ukizingatia sasa sayansi na teknolojia imerahisisha mambo.

Ni vizuri kila mmoja akatimiza wajibu wake kwa manufaa yetu wenyewe, na maendeleo ya Taifa letu kwa kuwa kila mmoja anayo haki ya kuwasiliana.

Ni kwa msingi huo, hata wagunduzi na watafiti wanaoshughulika na teknolojia mbalimbali waendelee kuhimizwa wazingatie mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Sada Amiri ni Mwandishi jijini Mwanza