Wanahabari tusione aibu kusafisha vyeti

Sunday December 8 2019

Wiki hii Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewakumbusha wanahabari wasio na stashahada kurudi shule kabla ya sheria ya Huduma za Vyombo vya habari 2016 kuanza kung’ata.

Lakini kuna jambo kubwa lililojificha nyuma ya pazia juu ya mwitikio mdogo wa wanahabari walioko makazini (practicing), kurudi shule nalo ni kukosa vyeti vya kidato cha nne.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mwandishi wa habari ni yule atakayekuwa amesajiliwa na bodi ya ithibati kwa ajili ya kukusanya, kuhariri na kusambaza habari kwenye vyombo vya habari.

Kanuni zilizotungwa baadaye na Waziri mwenye dhamana ziliweka kiwango cha chini cha elimu kwa mwandishi wa habari kuweza kukidhi kigezo cha kutambuliwa na bodi ni diploma.

Kifungu cha 50 (2) (b) cha sheria hiyo kinasema wazi mtu yeyote atakayefanya kazi ya uandishi wa habari pasipo kusajiliwa na bodi ya ithibati na kupewa “press card”, anatenda kosa la jinai.

Endapo atatiwa hatiani kwa kosa hilo atalipa faini isiyopungua Sh5 milioni na ambayo haitazidi Sh20 milioni au kutumikia kifungo kisichopungua miaka mitatu na kisichozidi miaka mitano.

Advertisement

Sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge mwaka 2016 na baadaye kusainiwa na Rais John Magufuli, ilitoa kipindi cha mpito kwa wanahabari wasio na sifa, kujiendeleza ili kufikia kiwango hicho cha elimu.

Bahati mbaya sana, pamoja na dhamira njema hiyo ya Serikali na wadau wa habari kuufanya uandishi wa habari kuwa ni taaluma inayoheshimika, mwitikio wa kurudi shule ni mdogo.

Kauli ya mkurugenzi mkuu wa TCRA, James Kilaba ni kukumbusha wanahabari kuwa suala la elimu kwenye tasnia hii halina mjadala, na kuwataka wasio na sifa kutumia muda uliobaki kusoma.

Nimeona ripoti ya TCRA kuhusu tathmini waliyofanya katika vyombo vya utangazaji nchini kwa maana ya radio na TV mwaka 2016/2017 ambayo inasema asilimia 90 hawakuwa na sifa.

Nimemsikia pia mkurugenzi wa Umoja wa Klabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Abubakar Karsan akisema amewasilisha mapendekezo serikalini kuhusu kusomesha wanahabari.

Pengine tatizo hili ni la kihistoria pia kwa kuwa hata katika andiko la Stummer (1998), anasema kutokana na sera ya soko huria miaka ya 90, vyombo vingi binafsi vilianzishwa Tanzania.

Idadi ya wanaofanya kazi ya habari wakaongezeka kutoka 600 mwaka 1992 hadi 3,000 mwaka 1996, lakini ni wachache tu miongoni mwao walikuwa wamepata mafunzo rasmi ya uandishi wa habari.

Wakati huo tulikuwa na vyuo viwili tu vya uandishi wa habari navyo ni Tanzania School of Journalism (TSJ) na Nyegezi Social Training Centre (NSTC) cha kanisa Katoliki.

Lakini sasa hivi Tanzania ina vyuo lukuki vinavyotoa mafunzo ya uandishi wa habari, lakini bado mwitikio wa wale wasio na sifa zinazotajwa na sheria kwenda kusoma ni mdogo na hauridhishi.

Sababu kubwa inayotajwa ni kwamba wengi wa waandishi walioko kazini ni wa kujitegemea, hawana kipato cha kuweza kujisomesha na vyombo vingi vya habari havitengi bajeti hiyo.

Inawezekana hiyo ikawa ni moja ya sababu, lakini iko sababu iliyojificha nyuma ya pazia, nayo ni waandishi wengi kuwa na vyeti vya kidato cha nne au cha sita ambavyo havina krediti.

Sifa za kujiunga na mathalan cheti cha kozi ya mawasiliano ya umma, kinataka mwombaji awe na angalau ufaulu wa D nne, lakini wapo wana D mbili, tatu au hata moja katika vyeti vyao.

Ukiacha kundi hilo, wapo wanahabari wenye astashahada na stashahada kutoka vyuo visivyotambuliwa na wengine wana astashahada na stashahada lakini vyeti vya sekondari vinakataa.

Sasa tunaweza kupiga kelele kuwa waandishi walioko kazini hawana uwezo wa kujisomesha, lakini kumbe kuna kikwazo kingine kimejificha nyuma ya pazia ambacho ni vyeti vya sekondari.

Waandishi wa aina hii wanatakiwa wajue kuwa hakuna njia ya mkato bali ni kurudi shule na kusafisha vyeti vyao ili waweze kupata sifa ya kujiunga na vyuo vya uandishi wa habari.

Wala tusione aibu kurudi shule na kusafisha vyeti kwa sababu wako ninaowafahamu, tena waandishi waandamizi sasa walipitia njia hiyo hiyo na wengine wana shahada sasa.