Wananchi Geita waunge mkono utafiti wa kaya maskini

Thursday February 8 2018Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel 

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel  

By Mwananchi

Gazeti hili toleo la jana lilikuwa na habari iliyohusu mpango wa Serikali wa kuzifanyia utafiti wa kipato na matumizi kaya maskini 608 za mkoani Geita ambao ni utekelezaji wa mwongozo wa mpango wa maendeleo wa Taifa, unaojulikana kama Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel alinukuliwa na Mwananchi akisema takwimu hizo zitasaidia Serikali na wadau wengine kutathmini hatua zilizofikiwa katika malengo ya kitaifa na kimataifa.

Gabriel alisema utafiti huo unatarajia kukusanya taarifa zinazohusu wanakaya, uzazi, unyonyeshaji, elimu na afya lakini watafiti pia wataangalia masuala ya uhamiaji, ulemavu, bima, ajira, biashara na mapato ya kaya, matumizi ya nishati, huduma za fedha na upatikanaji chakula, kilimo na mifugo.

Mbali na Gabriel, meneja takwimu mkoani Geita, Khalid Msabaha aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwa utafiti huo ni muhimu kwa mipango ya maendeleo. Azma ya Serikali ni kuwa nchi ya viwanda na kuona uchumi unatoka ulipo kwenda uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Tunafahamu katika utekelezaji wa dira hiyo, Serikali iliandaa mpango wa miaka mitano na kuweka vipaumbele vyake ambao ni miundombinu ya nishati, usafirishaji, Tehama, maji safi na maji taka na umwagiliaji.

Vipaumbele vingine ni kilimo cha mazao ya chakula na biashara, ufugaji, uvuvi, misitu, viwanda, hasa vinavyotumia malighafi ya ndani kwa maana ya kuongeza thamani, viwanda vikubwa vya mbolea na saruji, kielektroniki na maendeleo ya rasilimali watu, hasa kuinua stadi za kazi mkazo ukiwekwa katika masomo ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

Pia, Serikali imeweka mkazo katika kuimarisha mafanikio yatakayopatikana kutokana na utafiti wa kipato na matumizi katika kata 34 za mkoani Geita. Kwa maana nyingine utafiti huo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Kutokana na hoja hizo ni muhimu kwa wananchi wa mkoa huo kutoa ushirikiano utakaofanikisha lengo la Serikali, kwani maendeleo yoyote hayawezi kufikiwa bila kuwapo takwimu sahihi za walengwa katika maendeleo yao.

Ushirikiano wa wananchi katika utafiti huu ndiyo utatoa mwelekeo sahihi wa kutimiza malengo makuu ya kuifanya Serikali ifanikiwe kuifikisha Tanzania kwenye hadhi ya nchi zenye kipato cha kati na kuondokana na umaskini uliokithiri ifikapo 2025.

Tunafahamu malengo ya Serikali katika mpango huo ni kuwaletea wananchi maisha bora na mazuri, kudumisha uongozi bora na utawala wa sheria na kujenga uchumi imara wenye uwezo wa kukabiliana na ushindani.

Hata hivyo, rai yetu kwa watendaji wa Serikali wazingatie weledi katika utekelezaji wa jukumu lao la kufanya utafiti. Tunaamini hatutasikia kashfa ya kuwapo takwimu za kupika, wahusika watafika maeneo yote ya mijini na vijijini bila kujali changamoto za usafiri au fedha.

Kuendelea kwa Taifa la Tanzania kunategemea usahihi wa takwimu za kiwango cha umaskini nchini, kwa kuwa Serikali ipo katika mchakato wa utekelezaji wa mpango wa maendeleo ni wazi hakutakuwa na visingizio vya kukwamisha utafiti huo kwa asilimia 100.

Juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli za kuifanya Tanzania ya viwanda lazima ziungwe mkono kwa upatikanaji wa takwimu sahihi na kwa haraka za kiwango cha umaskini nchini.