MAONI: Wananchi wachukue tahadhari homa ya dengue

Saturday April 13 2019

Juzi Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema Watanzania 307 wamebainika kuugua ugonjwa wa dengue.

Kwa mujibu wa Waziri Ndugulile, wagonjwa waliobainika kuugua dengue kuanzia Januari hadi Aprili 2 ni kutoka Dar es Salaam yenye wagonjwa 252 na Tanga wagonjwa 55.

Waziri Ndugulile alisema ni ugonjwa unaoambukizwa na mbu aina ya aides ambao ni weusi na wenye madoa meupe yenye kung’aa.

Alisema dalili za dengue ni homa ya ghafla, kuumwa kichwa, hususan sehemu za macho, maumivu ya viungo, uchovu na kupata vipele vidogo.

Dalili nyingine zinazoweza kumtokea mgonjwa wa dengue ni kutokwa damu kwenye fizi na sehemu za uwazi za mwili mfano machoni, mdomoni, masikioni na sehemu za haja kubwa na ndogo.

Kwa kuzingatia dalili hizo aliwakumbusha wananchi kuchukua tahadhari ya ugonjwa huu unaoweza kuwa sababu ya mtu kupoteza maisha.

Ni vema wananchi wakachukua tahadhari kwa kuwahi hospitali ambako mgonjwa hupimwa damu kuangalia virusi na kupimwa kingamwili dhidi ya virusi hivyo.

Maelezo ya wataalamu wa tiba ni kwamba mpaka sasa hamna dawa kwa ajili ya ugonjwa huu ila dawa za kupunguza homa na maumivu huweza kutumika.

Dawa zinazotajwa na wataalamu hao ni paracetamol, kupumzika vizuri, kunywa maji lakini hali inapozidi inashauriwa kwenda hospitali.

Na kwa kuwa dalili zimewekwa wazi ni vyema kila mwananchi achukue jukumu la kwenda kupima ili kujua kama ana maradhi hayo au hana.

Tunalisisitiza hili tukiamini kwamba ingawa idadi ya wagonjwa 307 ni kubwa , huenda ikawa kubwa zaidi hasa kwa kuwa waliopimwa ni kutoka mikoa miwili tu, hivyo si ajabu kuna wagonjwa wengine mikoa mingine.

Kwa hiyo suala la kupima dengue lipewe nafasi yake na kuachana na ile dhana kwamba kila homa ni malaria na badala yake tunapojihisi uchovu au dalili zozote za homa ni muhimu kwenda kupima.

Zile tabia za kuhisi uchovu na kujenga dhana kwamba ni malaria au ugonjwa wowote na kuanza kujitibu bila vipimo ni hatari kwa kuwa mtu anaweza akadhani anajitibu kumbe anapoteza fedha na muda kwa tiba isiyo sahihi.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi ametahadharisha kuhusu matumizi ya dawa zenye diclofenac akisema kuwa si salama kwa mgonjwa wa dengue. Pia, ni muhimu kuepuka kuendelea kuumwa na mbu anayesambaza dengue.

Hii ni tahadhari muhimu inayotoa msisitizo huohuo kwa wenye kuamini kila homa ni malaria na kuvamia dawa zilizowahi kuwasaidia kupona siku za nyuma, hivyo wanapohisi homa au uchovu wanatumia dawa hizo hizo.

Watu hawa wanaweza kuwa wanaugua dengue na matokeo yake wanaongeza tatizo na hata kuhatarisha uhai wao kwa kutumia tiba isiyo sahihi.

Zaidi ya hilo pia ni muhimu kuangamiza mazalia yote ya mbu hasa kipindi hiki cha mvua, hii itasaidia kupunguza kama si kumaliza maambukizi ya dengue.