UCHAMBUZI: Wanaotupa taka ovyo wachuliwe hatua

Friday February 8 2019

 

Mabaraza ya mji na manispaa ya Zanzibar yanahitaji nguvu ya pamoja kumaliza tatizo la usafi wa mazingira katika maeneo yaliyopo karibu na madampo.

Hivi sasa imekuwa jambo la kawaida kupita maeneo hayo kukuta taka chini zikizagaa ilhali kumewekwa makontena maalumu kwa ajili ya kutupia taka.

Awali, ilikuwa ni jambo la ajabu kuona taka katika maeneo hayo zikizagaa ovyo chini ya makontena kutokana na kila mwananchi alitambua wajibu wake anaopaswa kutekeleza pindi akifikisha taka eneo hilo.

Hali hiyo ilitokana na taasisi husika yaani mabaraza ya mji na manispaa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuweka mazingira safi lakini pia usimamizi mzuri katika maeneo hayo ulikuwapo.

Awali, kitu kilichosababisha ustaarabu huo uwapo ni ule mpango wa mabaraza ya mji pamoja na manispaa kuanzisha utaratibu maalumu wa kupita mitaani kwa ajili ya kukusanya taka majumbani.

Utaratibu ambao kwa wakati wa kipindi hicho ulikuwa unafanyika vizuri, huku kila mwananchi aliitikia wito wa kuhifadhi taka zake vyema, hadi pale wanapopita wafanyakazi maalumu wa manispaa na kuchukua taka majumbani na kuzifikisha kwenye madampo.

Kiukweli jambo hilo lilikuwa zuri na liliweza kuleta faraja kwa jamii kuepuka maradhi ya mlipuko kama kipindupindu, lakini pia miji yetu ilikuwa inang’aa kutokana na uhifadhi wa taka kuwa mzuri na wa kupigiwa mfano.

Mpango wa kuchukua taka majumbani uliokuwa unafanywa na mabaraza ya manispaa ulikatika mwishoni mwa miaka ya 1990, kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ujenzi holela ambao ulisababisha baadhi ya matoroli ya kubebea taka kushindwa kupita mitaani tofauti na kipindi cha nyuma.

Baada ya ‘kufa’ kwa mfumo huo, Serikali iliandaa utaratibu wa kuwapo dampo maalumu za kutupia taka.

Licha ya nia njema hiyo ya Serikali kwa wananchi wake, lakini inaonekana kuna baadhi ya watu kwa makusudi wanapingana na utaratibu uliopo wa utupaji wa taka ndani ya makontena, hatimaye watu hao hutupa taka chini.

Wapo baadhi watu hujiona wana haraka ya kukimbilia kitu au kazi fulani, huku wengine hufanya hivyo kwa makusudi bila ya kujali afya za wananchi wenzao hasa wanaoishi maeneo ya karibu na madampo.

Pia, wakati mwingine makundi hayo hayo huonekana kuanzisha majalala sehemu zisizoruhusiwa kisheria kutokana na uvivu na ukaidi wao wa kufika maeneo yaliotengwa kwa ajili ya kutupa taka.

Ukweli ni kwamba hali hiyo hairidhishi hata kidogo, kwa kuwa inasababisha afya za wananchi kuwa hatarini kutokana na taka kuzagaa ovyo.

Ushauri wangu ni kwamba watu wanaokiuka taratibu za kutupa taka katika maeneo husika ni vyema wakachukuliwa hatua ili iwe fundisho kwa wengine wasiozingatia usafi.

Pia, hiyo itawasaidia wale wanaokaa jirani na madampo kutoandamwa na magonjwa.

Umefika Serikali, mabaraza ya mji, halmashauri na manispaa zote, kuhakikisha kwamba katika maeneo hayo kuna ulinzi maalumu ili kuyaweka mazingira safi.

Ni wazi kukiwa na ulinzi hakuna mwananchi ambaye atamwaga taka chini kinyume na utaratibu uliopo.

Pia kama kuna sheria za kuchukuliwa kuhusu wale ambao watabainika kwenda kinyume na utaratibu huo, umefika wakati sasa kuchukuliwa ili kuona mji na maeneo ya karibu na madampo yanaendelea kuwa na usafi kwa wakati wote.

Pia, ifahamike kwamba Zanzibar kama ilivyo miji mingine duniani, inahitaji kuwa safi.

Hata wananchi wake wanapaswa kuwa na afya bora kwa kuweka mazingira safi ili kuepuka magonjwa ya mlipuka kama kipindupindu.

Pia, wanapaswa kutekeleza maagizo ya Serikali hasa kutupa taka katika maeneo husika.

Jamii inapaswa kuelewa kuwa utupaji ovyo wa taka siyo kuikomoa Serikali, bali tunajikomoa wenyewe kwa kuwa tunajiweka katika hatari ya kupata magonjwa.

Ni vyema tukabadilika kwa kutunza mazingira yanayotuzunguka ili tuwe salama na magonjwa mlipuko hasa kipindupindu.

Uchambuzi huu umeandikwa na mwandishi wa gazeti la Mwananchi anapatikana kwa namba 0776 111915