UCHAMBUZI: Wanasiasa wajifunze kwa Zitto Kabwe

Muktasari:

  • Wanasiasa wa Tanzania hasa wabunge na madiwani wameweka rekodi ya kuacha nyadhifa zao tena walizozipata kwa gharama ya kodi za wananchi na kuliingiza Taifa kwenye gharama zingine za kufanya uchaguzi mdogo.

Hamahama ya wanasiasa wa vyama vya upinzani kukimbilia Chama cha Mapinduzi (CCM), siyo jambo geni tena masikioni mwa watu na hata wanahabari.

Wanasiasa wa Tanzania hasa wabunge na madiwani wameweka rekodi ya kuacha nyadhifa zao tena walizozipata kwa gharama ya kodi za wananchi na kuliingiza Taifa kwenye gharama zingine za kufanya uchaguzi mdogo.

Lakini kinachoshangaza zaidi ni wanasiasa haohao waliojiuzulu ubunge au udiwani wanagombea tena nyadhifa hizo kupitia chama kingine wanachojiunga nacho.

Yapo mengi yanazungumzwa kuhusu sababu za kuhama vyama vyao, lakini wenyewe wahamaji wanadai ni kuunga mkono juhudi za mamlaka ya chama tawala cha CCM. Lakini vyama vinavyokimbiwa na wanachama wake navyo vina madai yao ikiwamo madai ya watu wao kushawishiwa kwa fedha jambo ambalo hakuna mwenye uhakika nalo.

Watanzania hadi sasa wamekwishaumia kwa kodi zao kutumika kufanya uchaguzi mdogo tena wa kuwarejesha madarakani wabunge na madiwani waliojiuzulu nafasi hizo.

Mzigo huu wa gharama wanaobebeshwa na wale wanaojiuzulu nyadhifa hizo halafu uchaguzi unapoitishwa wanakuja kuzigombea tena kupitia chama kingine, unaacha maswali ya nini kiko nyuma ya pazia.

Lakini kinacholeta maswali zaidi ni pale anapoibuka kiongozi wa chama tawala na kuueleza umma unaobeba mzigo wa kurudia uchaguzi kwamba bado kuna kundi kubwa la wanasiasa wa upinzani wakiwemo wabunge na madiwani wanaotarajiwa kutimkia CCM.

Miongoni mwa maswali hayo ni je kama wapo wanasubiri nini hadi sasa? Safari yao ni ndefu kiasi gani hata wasifike? Kuna vitu hawajatimiziwa au kuna kazi waliyopewa hawajakamilisha? Kwa nini wanajulikana?

Eti wapo hata kwa idadi, wanajulikanaje hawa watu? Kwa nini wakirudi wanapewa nafasi za kugombea na pengine kupewa nafasi kubwa za kuitumikia nchi ilhali walishakuwa ‘ng’ombe waliokatwa mikia’ kama tulivyoelezwa.

Ama kweli inanikumbusha kauli ya mkongwe wa siasa na waziri wa serikali ya awamu ya kwanza, Balozi mstaafu Job Lusinde aliyewahi kuniambia katika mazungumzo ya kawaida miaka kadhaa iliyopita kuwa, “siasa siyo mchezo mchafu, bali ndani ya siasa kuna watu wanacheza rafu.”

Huu ni wakati wa kuwapambanua wanasiasa wa kweli na wanasiasa ‘matumbo’ ambao huelekeza matumbo yao upepo unakotokea na kisha ukigeuka wanageuka nao.

Haiwezi kuingia akilini kuwa, ukigombana na kiongozi wako ndani ya chama suluhisho ni kukihama na kujiunga na chama kingine. Je huko ukigombana pia utahama au utarudi nyuma?

Wengi wamerudi kule walikokimbia na kusema hakufai kutokana na haya na yale na walisimama katika majukwaa ya siasa wakairarua CCM, ajabu ni kwamba leo imekuwa dhahabu kwao.

Katika hili kuna kila sababu ya kujifunza na kuiga kwa kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo na mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ambaye anaendelea kujipambanua kuwa mwanasiasa na mpinzani wa kweli.

Zitto alipambana ndani ya chama chake alichokulia cha Chadema, aligombana na viongozi wa ngazi ya juu lakini alibaki na msimamo wake na kueleza ukweli wa mambo kuhusu alichokusudia kukifanya ndani ya chama, hata ukafika wakati akaamua kuachia nafasi yake na kuuachia ubunge wa Kigoma Kaskazini.

Katika misukosuko hiyo, vyama vingi vilimkodolea macho kwa kutaka ‘kumsajili’ katika timu zao wakiamini alikuwa ni mtu muhimu katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Zitto akionyesha ni mkomavu na mtu anayeishi kwa anachokiamini, pamoja na tetesi za ahadi lukuki alizokuwa anapewa, bado alisimama imara na kuonyesha siyo mtu wa kununuliwa na akaamua kuanzisha chama chake huku uchaguzi ukiwa umekaribia jambo ambalo ni gumu kufikia ndoto.

Bila ya kujali chama kingeweza kupata wafuasi na hata yeye kupata nafasi ya ubunge, lakini alisimama imara kwa miguu miwili na hadi anapita katika kilindi cha misukosuko bado anapambana akiwa upinzani.

Kama wangekuwepo akina Zitto wengi nchini, basi tungekuwa na CCM madhubuti ambayo Mwalimu Nyerere aliiacha kwani wangeona kuwa hakuna njia ya kuwachukua na hivyo chama tawala kingesimama imara zaidi.

Leo ni Zitto huyu ambaye ameanza kampeni za kuunganisha vyama ili kupata nguvu ya pamoja kwa ajili ya kushindana na chama tawala huku akiwa amepitia misukosuko mingi isiyokuwa na mfano wake.

Hamahama hiyo imewafanya hata CCM waondokane na utaratibu wao unaomtaka kila mwenye nia ya kugombea uongozi awe amedumu walau kwa miaka mitano ndani ya chama. Kwa sasa haipo kwani wanarudishwa leo na kesho wanateuliwa kugombea.Huu ndio wakati wa kufikiri itungwe sheria ya kuwataka wabunge na madiwani walazimike kubaki kwenye vyama vyao kwa kipindi chote cha ubunge au udiwani, hii itasaidia kuepuka gharama zisizo za lazima na kuwaepuka wanasiasa wasiokuwa na malengo ya maendeleo kwa Taifa.