UCHAMBUZI: Wanawake na matokeo kuongeza usawa kijinsia

Kuanzia Juni 3 hadi 6, Canada itaandaa na kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa katika kaulimbiu ‘Wanawake na Matokeo utakaofanyika katika jiji la Vancouver, British Columbia.

Ni mkutano mkubwa wa kimataifa utakaojikita katika kujadili masuala ya usawa wa kijinsia, afya, haki na ustawi wa wanawake na mtoto wa kike.

Tunatarajia washiriki zaidi ya 7,000 kutoka nchi zaidi ya 160 na wengine 100,000 wakiwamo wale ambao watakuwa wakifuatilia kwa njia ya mtandao.

Canada inajivunia uamuzi wa kuandaa na kuwa mwenyeji wa mkutano huu kwa sababu ‘Wanawake na Matokeo’ ni jukwaa linalofungua fursa nyingi. Ni zaidi ya mkutano.

Ni harakati za ulimwengu wote katika kuleta usawa wa kijinsia, shabaha ambayo inaweza kuleta tofauti katika vita vya kupigana na umaskini na kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya 2030.

Usawa wa kijinsia na kuwajengea uwezo wanawake na watoto wa kike huifanya jamii yoyote kuwa jumuishi, yenye amani na yenye ustawi. Canada inaunga mkono juhudi za kuleta usawa wa kijinsia nchini kwetu na duniani kote.

Nchini kwetu, tumechukua hatua za kuleta usawa wa kijinsia kwa kuwa na Baraza la Mawaziri ambalo kuna idadi sawa ya mawaziri wanawake na wanaume. Pia, bajeti ya mwaka 2018 ina mtazamo wa kijinsia na tulizindua mkakati kabambe wa kuzuia ukatili wa kijinsia.

Katika duru za kimataifa, tuna sera ya Canada ya kimataifa ya uwezeshaji wa kijinsia ambayo inazingatia usawa wa kijinsia katika masuala yote ya ushirikiano na nchi nyingine. Tunazingatia usawa wa kijinsia katika mikataba ya biashara huria na tunahakikisha kuwa kila sehemu ya jamii inafaidika kutokana na biashara na uwekezaji wa kimataifa.

Tunaendeleza maadili ya kimataifa na vitendo katika kujibu na kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike katika mitandao.

Kwa upande mwingine, watoto wa kike wanapokosa taarifa za masuala ya afya, uzazi na masuala ya mahusiano, wana uwezekano mkubwa wa kushindwa kuhudhuria shule, kukatisha masomo yao kutokana na ujauzito au kukabiliwa na magonjwa mbalimbali na ubaguzi.

Hapa Tanzania, tunafanya kazi na makundi mbalimbali ya wanawake ya kupigania haki za wanawake na hasa katika maeneo ya elimu ya uzazi na masuala ya mahusiano ya kimapenzi, pia katika vita vya kupinga ndoa za lazima na za utotoni na ukeketaji kwa wanawake.

Canada inafanya juhudi kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana nchini Tanzania wanapata fursa ya mafunzo kwa ajili ya ajira ambazo zinatokana na mahitaji, kupunguza vikwazo vya kijinsia ili kuingia katika soko la ajira na kuwasaidia kujenga maisha mazuri ya baadaye ya familia zao.

Katika ngazi ya kaya, wanawake wenye nguvu za kiuchumi huwa na kipato, uhuru, huweza kuwalea na kuwakuza watoto wenye afya na wenye elimu.

Moja ya vipaumbele muhimu kwa Canada ni kuhakikisha kuwa wasichana Tanzania wanapata elimu bora na endelevu. Ushahidi unaonyesha kuwa pale ambapo wasichana wanapewa elimu bora ya awali na wanapata msaada katika masomo yao, kuna uwezekano mkubwa wa kuhitimu masomo yao na kuongeza vipato vyao katika siku zijazo. Muhimu zaidi, kila ongezeko la asilimia 1 katika elimu ya mwanamke, huongeza pato la mwaka la uchumi kwa asilimia 0.2.

Tumepiga hatua kubwa sana Tanzania katika kuboresha mafunzo ya waalimu, kukarabati shule na vyuo vya waalimu, na kuhakikisha kuwa maelekezo ya elimu yanazingatia mahitaji maalumu ya watoto wa kike. Juhudi hizi zinachangia katika kukuza uchumi wa Tanzania na ujenzi wa Tanzania ya viwanda.

Canada kama mbia na rafiki wa Tanzania, huwashirikisha raia wake wote, asasi za kiraia, wafanyabiashara na viongozi wa kisiasa, ikiwaomba wafuate mfano wa Serikali ya Canada, na waongeze juhudi katika kujumuisha masuala ya usawa wa kijinsia katika mipango yao yote.

Katika miezi ya hivi karibuni, tumekuwa na jitihada na matukio mbalimbali katika jiji la Dar es Salaam kuongeza ufahamu wa suala zima la “Wanawake na matokeo 2019”.

Ni matumaini yetu kuwa kupitia matukio haya washiriki wa mkutano kutoka Tanzania watakuwa katika nafasi nzuri kueleza mtazamo na dira ya Tanzania katika Jiji la Vancouver na kujenga ushirikiano mzuri na wadau mbalimbali kutoka katika nchi mbalimbali za dunia.

Pamela O’Donnell ni Balozi wa Canada nchini Tanzania