Wataalamu: Saratani ya tezi ikiwa hatua za awali inatibika

Friday February 8 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Saratani ya matezi (Hodgkin’s Lymphoma) huathiri matezi yalipo katika mwili wa binadamu hasa ya makwapa, shingoni na kifuani.

Matezi yaliyoshambuliwa huweza kusambaa kwenye matezi mengine mwilini hasa kwenye bandama (spleen) iwapo mgonjwa hatapata matibabu.

Miongoni mwa waliowahi kuugua saratani ya matezi ni Maimuna Salehe ( 25) mkazi wa Kondoa mkoani Dodoma ambaye anasema : “Muda mfupi baada ya kujifungua mtoto wangu wa kwanza, nilianza kuumwa, nilienda hospitali nikapewa dawa nikapata nafuu, lakini baada ya muda niliona tumbo langu linajaa utafikiri nina mimba nyingine, ndugu na wifi zangu walinishangaa sana kwa hali niliyokuwa nayo.”

Anasema baada ya kuona hivyo, alirudi tena hospitali na kufanyiwa vipimo zaidi na kugundulika kuwa na saratani ya matezi.

“Awali nilijua kuwa nina tatizo la kifua kikuu lakini baada ya kufanya vipimo zaidi, niligundulika kuwa na saratani ya matezi na kuanza matibabu haraka,” anasema Salehe ambaye aligundulika kuwa na tatizo hilo, mwaka 2016 na sasa amepona na anaendelea na kazi zake.

Daktari bingwa wa saratani kutoka kliniki ya Besta Super Specialized Polyclinic, Yemela Ndibalema anasema aina hiyo ya saratani huchanganywa na ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) unaoathiri matezi na mara nyingi mtu anaweza kutibiwa kama mgonjwa wa TB bila kupata nafuu, lakini kumbe ana saratani ya matezi.

Anasema neno ‘Hodgkin’s limetokana na jina la mwanasayansi maarufu ambaye aligundua saratani hii mwaka 1832.

Jina lake alikuwa akiitwa Thomas Hodgkin, hivyo kwa heshima yake, ugonjwa huu ukaitwa Hodgkin’s Lymphoma.

Dk Ndibalema anasema saratani hii huanzia kwenye mfumo wa matezi na kusambaa sehemu nyingine za mwili mfano katika mfumo wa damu na katika ute uliopo katika mifupa (Bone Marrow).

Anasema kuna matezi ambayo huvimba kutokana na maambukizi au sababu mbalimbali hasa kuwapo wadudu wa TB, lakini baada ya muda au matibabu sahihi, matezi hayo huisha kabisa.

“Ukiona matezi yanaendelea kuvimba wakati upo kwenye matibabu kwa zaidi ya wiki mbili hadi mwezi, ni vyema kurudi hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi, huenda hizo ni dalili za saratani ya matezi,” anasema Dk Ndibalema.

Anabainisha saratani ya matezi inashika nafasi ya tano kati ya saratani 10 zenye wagonjwa wengi nchini huku walio katika hatari ya kupata tatizo hilo ni vijana wenye kati ya miaka 25 hadi 30 na watu wazima wenye miaka kuanzia 50 na huwapata zaidi wanaume kuliko wanawake.

Dalili za saratani ya matezi

Anasema dalili ya saratani hii ni kuvimba matezi na kupata homa mara kwa mara pamoja na kuwa na upungufu wa damu.

Dalili nyingine ni mwili kuchoka, kutoka jasho lililopitiliza, kupungua uzito ndani ya kipindi kifupi na kuvimba matezi ambayo hutengeneza vidonda.

Anasema kuvimba sana kwa matezi ya shingoni na ndani ya kifua inaweza kusababisha kukandamiza na kubana mshipa mkubwa wa damu (superior vena cava) na kuvimba uso na shingo pamoja na kushindwa kupumua vizuri, kitaalamu inajulikana kama superior venacava syndrome.

“Mara nyingi mgonjwa anakuwa amevimba matezi kwenye maeneo ya shingo na makwapa, lakini uvimbe unaweza pia kujitokeza kama mtoki. Kama mgonjwa asipogundulika na kupata matibabu mapema, uvimbe unaweza kusababisha mtu kivimba uso na mikono au miguu,” anasema Dk Ndibalema.

Aina za saratani za matezi

Dk Ndibalema anasema kuna aina mbili za saratani za matezi ambazo ni Hodgkin’s Lymphoma na Non-Hodgkin’s Lymphoma

“Baada ya Thomas Hodgkin’s kuielezea aina hii ya saratani, mwanasayansi mwingine Reed Sternberg katika utafiti wake aligundua kuwa, ukichukua kinyama kutoka kwenye tezi la mgonjwa, kuna aina ya seli maalumu zinazoonekana kwenye darubini kwa wagonjwa mwenye saratani ambayo Thomas Hodgkins aliielezea, lakini aina hii ya seli haionekani kwa wagonjwa wengine,” anabainisha Dk Ndibalema.

Anafafanua kuwa baada ya utafiti zaidi, ikagungulika kuwa uwapo wa aina hii maalumu ya seli unazifanya saratani za matezi kuwa tofauti kwenye matibabu, hivyo kwa ugunduzi huo, seli hizi zilipewa jina la mgunduzi na kuitwa Reed Sternberg seli (Reed Sternberg cells- RB-cells).

Hivyo, saratani zenye uwapo wa RB-cells ndiyo zinaitwa Hodgkins Lymphoma na zile ambazo hazina RB-cells zikapewa jina la Non Hodgkins Lymphoma.

Dk Ndibalema anasema utofauti huo unafanyika hospitali baada ya kinyama kuchukuliwa kutoka kwenye tezi iliyoathirika na kwenda kufanyiwa uchunguzi maabara .

Nini kifanyike

Mkurugenzi wa Chama cha Uzazi na Malezi bora nchini (Umati), Dk Lugano Daimon anasema ni wakati kwa jamii kubadilisha mfumo wa maisha kwa kuzuia ulaji usiofaa lakini pia kuwa na utaratibu wa kufanyia uchunguzi afya zao mara kwa mara ili kuepuka magonjwa.

“Lakini, tunasisitiza mionzi inatakiwa itumiwe kwa umakini na uangalifu mkubwa,” anasema Dk Daimon.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anasema ikatika kila wagonjwa 100 wa saratani, 34 kati yao ni wa saratani ya mlango wa kizazi, wagonjwa 12 ni wa saratani ya matiti.

Pia, anasema katika kila wagonjwa 100, wagonjwa 80 wanafika hospitali wakiwa katika hatua ya tatu na nne, hivyo kupona kwao kunakuwa ni kugumu.