MAONI: Wateule wapya fanyeni kazi, wekeni siasa pembeni

Wednesday August 8 2018

 

Wakuu wapya wa mikoa na wilaya walioteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli wameripoti katika vituo vyao na tayari wameanza kazi. Wakuu hao kwa maana nyingine ni wawakilishi wa kiongozi huyo mkuu wa nchi katika maeneo wanakofanyia kazi na ndio viongozi wa juu kabisa katika sehemu hizo wakiongoza kamati za ulinzi na usalama.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 61 (4), bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (5), kila mkuu wa mkoa atakuwa na wajibu wa kusimamia utekelezaji wa kazi na shughuli zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika mkoa aliokabidhiwa.

Ibara hiyo inaendelea kusema kuwa, “na kwa ajili hiyo, atatekeleza kazi na shughuli zote zilizotajwa na sheria, au kwa mujibu wa sheria kama hizi au shughuli za mkuu wa mkoa na atakuwa na madaraka yote yatakayotajwa na sheria yoyote iliyotungwa na Bunge.”

Kwa maana ya kipekee kabisa, wakuu wa mikoa ni viongozi waliopewa madaraka makubwa katika nchi yetu. Wamepewa dhima kubwa kwani mamlaka yao yanagusa katika kila eneo lililopo kwenye maeneo yao ya kiutawala. Vivyo hivyo kwa wakuu wa wilaya, maana nao wanasimamia kila jambo katika wilaya wanazoziongoza.

Wakati tunawapongeza kwa mara nyingine kwa kuteuliwa kwao kuteketeleza majukumu ya kikatiba waliyokabidhiwa katika kulitumikia Taifa letu, tunapenda kuwaasa kufanya kazi kwa bidii wakiongozwa na sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.

Tunasema hivyo tukiwakumbusha tu kuwa, wajibu waliokabidhiwa unalindwa na misingi ya sheria. Ni jambo zuri kufanya kazi katika misingi inayotambuliwa na sheria na ni vyema kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia sheria inavyowataka.

Hata hivyo, wapo baadhi ya watendaji wa Serikali wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya ambao hili la kutimiza wajibu wao kwa kufuata sheria bila kuingiza siasa linakuwa gumu, badala yake wamekuwa wakiingiza masuala ya kisiasa hata katika mambo yasiyohusiana nazo.

Ni kutokana na utendaji wa aina hiyo, wamekuwa wakisababisha mikwaruzano isiyokuwa na maana na wananchi, hasa pale inapotokea kwamba wanayoyasema au kuyatenda kisiasa yanakwenda kinyume na misingi ya utumishi wao na kupokewa kwa hisia tofauti ndani ya jamii.

Ni vyema sasa, kwa pamoja wakuu wa mikoa na wilaya wapya pamoja na waliopo wakajikita kutimiza majukumu yao kwa kufuata misingi ya sheria za kazi zao, badala ya kuonekana kuwa wanasiasa zaidi, huku majukumu yao ya kikatiba wakiyaweka kando.

Kwa mtumishi wa umma anayesimamia misingi ya haki na kwa mujibu wa sheria, siku zote utumishi wake hutukuka na hilo ndilo muhimu, lakini kwa wanaokwenda kinyume na hilo, hata wanapoondolewa au kuondoka kazini, basi jamii hufurahia kwa sababu ya kuendekeza kwao mambo yasiyopendeza.

Hizi siasa zinazolalamikiwa na wananchi kufanywa na baadhi yao wawaachie wanasiasa, wao wafanye kazi, wasimamie haki na watimize wajibu wao kwa mujibu wa Katiba.