UCHAMBUZI: Wazazi Kisarawe, msimuangushe DC Jokate

Kelele nyingi kuhusu mimba za utotoni zimepigwa lakini hadi sasa changamoto hiyo imeendelea kuitafuna jamii ya watanzania.

Ni kawaida kwa watoto wengi kuandikishwa darasa la kwanza ila si wote wanaofanikiwa kumaliza masomo yao hadi darasa la saba au kidato cha nne kwa sababu ya kupata ujauzito.

Licha ya kuwa zipo sababu nyingi zinazowafanya watoto wa kike hasa kutoka familia maskini kupata ujauzito na kukatisha masomo yao, wazazi na jamii kwa ujumla ina mchango mkubwa katika suala hili.

Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo alitoa msimamo mkali katika kipindi chake cha uongozi kuhusu suala la wanafunzi kupata mimba.

Anasema uongozi wa halmashauri hiyo haitowavumilia watendaji na wazazi wanaowaficha wanafunzi wanaopewa ujauzito na kusababisha wahusika kuendelea kuwa huru kwa kukosekana ushahidi.

Jokate anasema watakaobainika kufanya michezo hiyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao bila kujali mamlaka na vyeo walivyonavyo ndani ya chama na Serikali.

Kauli hii imekuja kufuatia kuwapo kwa kesi nyingi za watoto kupewa ujauzito lakini zinaishia kufutwa kutokana na kukosekana ushahidi, hiyo yote ikichangiwa na wazazi na viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa.

Kitendo cha wazazi kuamua kumalizana nyumbani na watu wanaowapa mimba mabinti zao ni kikwazo kikubwa katika vita hii na kuchangia tatizo hili kuonekana kawaida.

Ninavyosema kawaida namaanisha kawaida, binti anapewa ujauzito, mzazi anamfuata mhusika au familia ya mhusika inakwenda nyumbani kwa binti na kulimaliza kwa mazungumzo au wakati mwingine fedha kidogo.

Huo ndiyo unakuwa mwisho wa ndoto ya binti kupata elimu, huku aliyempa ujauzito akiendelea ‘kudunda’ na maisha yake, wazazi nao wakila punje mbili tatu walizopewa.

Kwa Kisarawe hilo limefika mwisho, Jokate ameahidi kuwa mapambano yake yataanzia kwa viongozi wa vijiji, vitongoji na kata hadi kwa wazazi ambao wataruhusu mabinti zao wakatishe masomo kutokana na mimba halafu wahusika wasifikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Binafsi naunga mkono harakati hii ambayo nina uhakika itakwenda kusaidia watoto wa kike katika wilaya ya Kisarawe kupata elimu.

Hakuna mwanajamii asiyefahamu kuhusu suala hili ingawa huenda wengi hawafahamu ukubwa wa tatizo, ukweli ni kwamba bado kuna watoto wengi wa kike wanakatisha masomo kwa sababu ya mimba.

Kinachoshangaza zaidi kwamba sheria ipo wazi na inaelekeza kabisa ni adhabu gani anastahili kupewa mtu anayempa ujauzito mwanafunzi, lakini vitendo bado vinaendelea.

Watu wanatambua hilo na ndiyo sababu wanaamua kuwatumia wazazi kumaliza masuala hayo nyumbani na kuficha ushahidi ili sheria isifuate mkondo wake.

Wazazi nao kutokana na ugumu wa maisha na ujirani wanaona bora wawageuze mabinti zao kuwa mtaji wachukue kitu kidogo kutoka kwa familia ya washtakiwa bila kujua wanapigilia msumari wa kuharibu maisha ya watoto wao.

Sasa tumeanza mwaka mpya hata fikra zetu zinapaswa kuwa mpya, hatutaki kuona upuuzi huu unaendelea watoto wote wanatakiwa kumaliza masomo yao kama walivyoanza na ikitokea amekatisha sababu iwe ni kifo sio mimba.

Ujumbe wangu kwenu wazee, wazazi, viongozi wa vijiji na kata katika Wilaya ya Kisarawe, jitihada kubwa zinafanyika kuhakikisha kiwango cha elimu kinaunuliwa katika wilaya yenu basi na nyie muwe sehemu ya jitihada hizo.

Hakikisheni watoto wanasoma na wanasoma kweli kwani urithi pekee wa mtoto ni elimu, kwani hata familia ikiwa na mali bila elimu huyo mtoto hatoweza kuziendesha pindi zitakapokuwa mikononi mwake.

Anayesababisha mimba hiyo anastahili adhabu kali kwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria hata kama ndiye ametuletea maji kwenye kijiji chetu ndiye mwekezaji anayetoa ajira kwa vijana wengi.

Wito wangu kwa viongozi mnapaswa kutambua kuwa uongozi ni dhamana, mliaminiwa ndiyo sababu mkapewa nafasi hivyo. Itumikieni jamii iliyowaamini na siyo kurubunika kwa vijisenti huku mkiwaacha watoto wa kike wanaangamia.

Elizabeth Edward ni mwandishi wa gazeti hili anapatikana kwa barua pepe [email protected]