Zipi dalili hatari kwa watoto?

Friday January 18 2019Dk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

Zipo dalili na viashiria ambavyo ni kielelezo kuwa mtoto anaumwa sana (ana ugonjwa mkali).

Dalili hizi zimegawanywa sehemu kuu mbili yaani dalili za hatari na dalili zinazohitaji kupewa kipaumbele.

Baadhi ya wazazi au walezi wasio na ufahamu wamekuwa wakichukulia kuwa ni dalili za kawaida na kuchelewa kufanya uamuzi ya kumpeleka mtoto mapema katika huduma za afya.

Inapotekea mtoto mwenye dalili za hatari akacheleweshwa kufika katika huduma za afya huweza kupoteza maisha au kupata madhara ya muda mrefu.

Ni muhimu kwa wazazi na walezi kuzijua dalili hizi ili pale atakapoziona zimejitokeza kwa watoto wao wawahi kufika katika huduma za afya mapema.

Ikitokea mtoto anashindwa kunyonya kabisa au kunywa chochote hata ukimlazimisha inashindikana, hii ni moja kiashiria kwamba mtoto ana ugonjwa mkali.

Mtoto anapokuwa na ugonjwa wowote mkali ikiwamo maralia kali, nimonia kali, uti wa mgongo mara nyngi dalili hii hujitokeza.

Mtoto kutapika kusiko kwa kawaida huku akitoa kila kitu alichokula, vile vile akawa anatumia nguvu nyingi huku matapishi yakitoka kwa msukumo mkubwa.

Hii ni moja ya dalili inayoashiria mwili kushambuliwa na ugonjwa mkali. Unapoona ametapika kwa namna hii mpeleke katika huduma za afya haraka.

Kupatwa na degedege ni dalili inayoashiria uwapo wa ugonjwa mkali unaoathiri mfumo wa fahamu ikiwamo ubongo.

Pale anapoona mtoto amepatwa na degedege fahamu ni tatizo la kiafya na si vinginevyo.

Magonjwa kama malaria, nimonia, jeraha la ubongo, uti wa mgongo, uwepo wa vimelea katika damu, upungufu wa sukari mwilini na chumvi chumvi huwa na madhara ya kiafya yanayoweza kusababisha degedege.

Mtoto anaweza kukosa nguvu na kuwa mlegevu kupita kiasi mpaka kupoteza fahamu au kuweweseka.

Mwandishi wa makala haya ni daktari