Mongella atoa siri ya wakopaji kuaminiwa na taasisi za fedha

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella

Muktasari:

Aliyasema hayo juzi wakati akizundua tawi la Benki ya BancABC jijini Mwanza, huku akitoa wito kwa wakazi kujenga utamaduni wa kukopa katika benki ili kukuza biashara zao na kukamilisha kwa wakati miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema siri ya mafanikio ya mikopo ni kutimiza malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa wakati, ili kujiweka katika nafasi ya kuendelea kuaminiwa na taasisi.

Aliyasema hayo juzi wakati akizundua tawi la Benki ya BancABC jijini Mwanza, huku akitoa wito kwa wakazi kujenga utamaduni wa kukopa katika benki ili kukuza biashara zao na kukamilisha kwa wakati miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mongella alisema ujio wa tawi hilo ni wakati mwafaka kwa kuwa Mwanza ni moja ya miji inayokuwa kwa haraka nchini, hivyo huduma za benki zinahitajika ili kuwawezesha wananchi kupata mitaji kwa ajili ya biashara na shughuli mbalimbali.

“Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza BancABC kwa kuona umuhimu wa kuleta huduma kwa kufungua tawi jipya. Naamini bado kuna watu wengi ambao hawajanufaika na huduma za benki hivyo ni imani yangu mtafanya kazi kwa bidii ili kuwafikia wananchi na wafanyabiashara wengi mjini na vijijini katika ukanda huu wa ziwa,” alisema.

Mongella alionyesha kufurahishwa na hatua ya benki hiyo ya kupunguza riba.

“Hii itawavutia wafanyabiashara wengi hivyo kukuza biashara zao na kuwekeza katika miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa majengo ya biashara na nyumba za makazi. Upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu, utasaidia kuboresha hali ya maisha ya wakazi wa Mkoa wa Mwanza,” alisema.

Mongella alizitaka taasisi nyingine za fedha kuangalia uwezekano wa kupunguza riba zao ili kuwafanya Watanzania wengi kuweza kukopesheka.

“Ni ukweli usiopingika riba kubwa imekuwa kikwazo kikubwa kwa wakopaji,” alisema.

Naye mkurugenzi mtendaji wa BancABC Tanzania, Dana Botha alisema uzinduzi wa tawi hilo ni sehemu ya mpango mkakati wao wa kupeleka huduma za benki karibu na wananchi na wataendelea kufungua matawi zaidi nchini.