Panya wavamia mashamba ya mpunga, mahindi

Thursday January 18 2018

 

By Lilian Lucas,Mwananchi [email protected]

       Morogoro. Zaidi ya eka 350 za mpunga na mahindi Wilaya ya Kilombero mkoani hapa zimeharibiwa na panya baada ya panya hao kuingia kwa kasi shambani na kula mazao hayo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Denis Londo akizungumza na mwandishi wa Mwananchi alisema tatizo hilo la panya kushambulia mazao limeleta hasara kwa wakulima wengi wanaotegemea mazao hayo kwa biashara na chakula.

Alisema panya hao walianza uharibifu huo Novemba 2017 baada ya kuonekana Tarafa ya Mngeta kata za Chita, Melela na Mwaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.

Pia, alisema walionekana katika kata nyingine za Halmashauri ya Mji wa Ifakara.

Londo alisema juhudi za halmashauri hizo mbili katika kuwadhibiti panya hao zilifanikiwa.

Alisema halmashauri hizo ziliamua kununua sumu na kuwateketeza panya hao japo kuna baadhi ya maeneo bado wanaendelea kusumbua.

Mkurugenzi wa Mji wa Ifakara, Francis Ndulane alisema baada ya kupata taarifa mapema mwezi huu aliungana na mkurugenzi mwenzie wa Halmashauri ya Kilombero kuhakikisha udhibiti wa panya hao unaendelea kufanyika kwenye maeneo yote ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano na wananchi.

Ndulane alisema katika halmashauri yake ya mji mdogo wa Ifakara maeneo yaliyoathirika ni vijiji vya Idete, Ihanga na Lumuma.

Mkurugenzi huyo wa mji alisema kwamba katika ununuzi wa sumu ya panya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero walinunua kilo 50 na halmashauri ya mji walinunua kilo 10.

Alifafanua kuwa kazi ya usambazaji wa sumu hiyo ilianza na maeneo mengi wamefanikiwa kuwaangamiza.

“Kwa sasa wataalamu wa kilimo katika halmashauri zote wanasambaza sumu maeneo yote yaliyoathirika na pia wanahamasisha wakulima kutumia njia za kienyeji ili kuwadhibiti panya hao kwa namna moja au nyingine, tunashukuru zoezi linafanyika vyema,” alisema.

Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Mohamed Ramadhani alisema kwa sasa hali ni shwari katika maeneo mengi wilayani humo kwa kuwa walianza kugawa sumu tangu Januari 6.

Alisema panya hao walianza kufanya uharibifu Septemba na Oktoba 2017.     

Advertisement