Profesa Silayo afuata nyayo za Waziri Mkuu, naibu waziri

Thursday January 11 2018

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo (kushoto) akimwelekeza Diwani wa Kata ya Ulaya iliyopo wilayani Kilosa, Matokeo Kennedy namna bora ya kupanda mche wa mti baada ya kuutoa kwenye bustani ya miti ya TFS wilayani humo. Picha na Mpigapicha Wetu. 

By Tulizo Kilaga, Mwananchi [email protected]

Mtendaji mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo ametoa hadi mwisho wa mwezi huu wananchi waliovamia Msitu wa Hifadhi wa Ukwiva kwa ufugaji, makazi pamoja na shughuli zingine za kibinadamu kuondoka na watakaokaidi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Agizo hilo la Profesa Silayo limetia mkazo katika amri iliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoitoa Juni, 2017 akiwataka wananchi wanaoishi na kufanya shughuli zao kwenye maeneo ya hifadhi za misitu na vyanzo vya maji kuhama kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.

Vilevile, agizo kama hilo lilitolewa na naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga alipotembelea na kukagua mipaka ya msitu wa Kazimzumbwi wilayani Kisarawe mwishoni mwa mwaka jana aliyesisitiza atakayekaidi abanwe kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza kwenye mkutano na viongozi wa Kijiji cha Nyameni wilayani hapa, Profesa Silayo aliwataka wawaambie wavamizi wahame kwenye eneo la hifadhi kabla Serikali haijaanza kuchukua sheria kwa kuwa eneo hilo lilishapimwa miaka mingi na mipaka yake inatambulika kisheria.

“Ndugu zangu najua wavamizi wa hifadhi hii wanakuja kupata mahitaji yao kwenye kijiji hiki na wengine mnawajua sasa nawaagiza muwaambie waondoke mara moja, nilishaongea na DC kwamba kufikia mwisho wa mwezi huu wote wawe wameondoka, watakaokaidi waondolewe kwa nguvu,” alisema.

“Nitoe wito kwa wavamizi wote ambao wako ndani ya Msitu wa Hifadhi wa Ukwiva wawe wameondoka ndani ya siku hizi takriban 20 zilizobaki na wakiwa wanatoka wanakijiji wawape ushirikiano ili kusiwepo na upotevu wa amani kati ya wakulima na wafugaji.”

Diwani wa Kata ya Ulaya, Matokeo Kennedy alisema wamepokea maelekezo kutoka kwa mkuu wa wilaya akiwataka watengeneze mazizi ili kuhifadhi ng’ombe pindi operesheni itakapoanza.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi aliwataka wanaoishi kwenye misitu na vyanzo vya maji kutojidanganya kuandaa rushwa ili waachwe kwenye maeneo waliyovamia kwa kuwa hawataachwa.     

Advertisement