Vertif yaingiza UPS kukabili kukatika umeme viwandani

Muktasari:

  • UPS hizo zenye uwezo wa kutunza chaji kwa zaidi ya saa 24, hutoa taarifa ya hatari yoyote inayoweza kutokea saa nane kabla ili wahusika wajiandae namna ya kukabiliana nayo.

 Ili kuepuka hasara zitokanazo na kukatika kwa umeme mara kwa mara, kampuni ya Vertif imeingiza nchini vifaa vya kutunzia umeme (UPS) kwa ajili ya taasisi na viwanda.

UPS hizo zenye uwezo wa kutunza chaji kwa zaidi ya saa 24, hutoa taarifa ya hatari yoyote inayoweza kutokea saa nane kabla ili wahusika wajiandae namna ya kukabiliana nayo.

Mfanyabiashara mwenza wa kampuni hiyo, Mihayo Willmore alisema vifaa hivyo vimefanyiwa maboresho kukabili dharura na sintofahamu zinazoweza kutokea na kusababisha hasara kwa wamiliki wa viwanda au taasisi kubwa.

“Tumelenga sekta za afya, viwanda, vituo vya kanzidata na taasisi za Serikali ambazo mara nyingi zinahitaji umeme wa ziada katika utendaji wake,” alisema.

Willmore alisema UPS hizo ni nyenzo ya kunusuru uzalishaji viwandani au uhudumiaji wagonjwa kwa maelezo kwamba ndani ya saa 24, wahusika watakuwa wamejipanga kutafuta suluhu ya uhakika.

“Inategemea na matumizi lakini UPS hizi zina uwezo mkubwa wa kutunza chaji hivyo kufaa inapotokea dharura umeme ukakatika au jenereta likagoma kuwaka hivyo kutoa muda wa kutosha kutatua tatizo,” alisema Willmore.

Naye mkurugenzi wa kampuni hiyo Kusini mwa Afrika, Johan van Wyk alisema umeme umekuwa ni tatizo kubwa katika nchi nyingi duniani, hivyo UPS hizo zitakuwa msaada.

“Wateja wetu wanasema UPS hizi zimewasaidia kuepuka madhara ambayo yangeweza kuwapata kila umeme unapokatika,” alisema Wyk.