Saida Karoli kuwasha moto Sauti za Busara

Muktasari:

  • Burudani hiyo yenye hadhi ya kimataifa hufanyika katika eneo la Ngome Kongwe na Bustani ya Forodhani, ikiwa na maonyesho 46 kutoka kwa wanamuziki 400

Mwanamuzi wa nyimbo za asili, Saida Karoli atakuwa miongoni mwa wanamuziki zaidi ya 400 watakaotumbuiza kwenye Tamasha la Muziki la Afrika Mashariki, Sauti za Busara katika maadhimisho yake ya miaka 15  katika Mji wa Stone Town, Zanzibar kuanzia Februari, 8 hadi 11, 2018.

Tamasha hilo litashuhudia kuzaliwa ‘upya’ kwa mwanamuziki, Saida Karoli kwenda katika ngazi ya kimataifa, Saida amerejea katika nafasi yake kwa kishindo kikuu katika mwaka 2017 baada ya kukaa nje ya muziki kwa muda.

Katika tamasha hilo litashudia wigo mpana wa wasanii na vikundi mbalimbali vya muziki vinavyotambulisha tamaduni tofauti tofauti za Kiafrika, tamasha hili aghalabu limejipambanua kuwa miongoni mwa jukwaa ambalo nyota wa Afrika wanaonyesha nguvu ya ubunifu wao katika mandhari ya kipekee iliyowahi kutumika tangu karne zilizopita.

Burudani hiyo yenye hadhi ya kimataifa hufanyika katika eneo la Ngome Kongwe na Bustani ya Forodhani, ikiwa na maonyesho 46 ya kusisimua, ikiwakusanya kwa pamoja wasanii zaidi ya 400 katika majukwaa matatu tofauti ndani ya siku nne katika mwezi wa Februari.

Watanzania na wageni wa mataifa mbalimbali kutoka katika kila kona ya dunia husubiria kwa hamu tamasha hili lenye kusisimua na linalotoa fursa ya kuona vipaji vya aina mbalimbali vya wanamuziki ambao ni gumzo Afrika na nje ya Afrika.

Kama ambavyo wengi wameshaelezea kuhusiana na tamasha hili, tamasha la mwaka huu ni la kipekee kwa kuweza kukusanya orodha ya wasanii bora kuwahi kutokea, likichanganya vipaji vinavyochipukia pamoja na wale wakongwe kutoka katika nchi za jirani na zile za mbali, wakidumu katika lengo moja la “Kuunganishwa na Muziki”

Tamasha hili linawakilisha utamaduni tofauti tofauti wa Kiafrika kutoka katika vikundi mbalimbali vya nchi kama vile Algeria, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Misri, Kenya, Malawi, Morocco, Rwanda, Senegal, Afrika Kusini, Uganda na Zimbabwe.

Tamasha limepiga hatua mbele kutoka pale ambapo lilikomea katika maadhimisho ya awamu ya 14, kwani orodha hiyo pia inajumuisha sauti za kipekee za wanamuziki kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, ambapo vikundi 15 vipo tayari kwa ajili ya kuionyesha dunia utajiri wa muziki wa nyumbani.

Makundi mengine ni pamoja na Kasai Allstars (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), Zakes Bantwini (Afrika Kusini), Somi (Uganda / USA), Msafiri Zawose (Tanzania), Ribab Fusion (Morocco), Kidum & the Boda Boda Band (Burundi / Kenya), Mlimani Park Orchestra (Tanzania).

Pia katika orodha hiyo wapo wanamuziki kama vile Grace Matata (Tanzania), Mohamed Ilyas & Nyota Zameremeta (Zanzibar), Makadem (Kenya), Diana Samkange ‘MaNgwenya’ (Zimbabwe), Fatma Zidan (Misri / Denmark), Inganzo Ngari (Rwanda).

Wengine ni Segere Original (Tanzania), Simangavole (Reunion), Maia & the Big Sky (Kenya), Kiltir (Reunion), El Dey (Algeria), Simbin Project (Senegal / Uswisi), CAC Fusion (Tanzania), Mbanaye (Malawi), Ernest Ikwanga (Malawi) na Isack Abeneko (Tanzania).

Ili kudumu katika utamaduni wa kweli za Tamasha la Sauti za Busara, vikundi vyote vitafanya maonyesho yao mubashara, kwa kushuhudia onyesho la kwanza likifanyika katika viwanja vya  Kisonge kabla ya Gwaride la Carnival halijafanyika kuashiria kuanza kwa onyesho lenye hadhi ya kidunia linalochukua siku nne katika majukwaa matatu.

 Mkurugenzi wa Tamasha hili, Yusuf Mahmoud alivyoeleza hivi karibuni kuwa, “Muziki ni lugha ya ulimwengu mzima, ambapo kupitia huo (muziki) dunia inaitazama Afrika katika mtazamo chanya; Afrika ni mahiri, Afrika ni  tajiri katika tamaduni zake nyingi na maelezo yake. Tunahitaji kujenga daraja la amani na umoja kwa dunia nzima; ni njia ipi bora ya kujenga daraja hili zaidi ya  kupitia lugha yetu moja ya ulimwengu ambayo ni muziki?”

Tamasha la Sauti za Busara linatoa ofa ya kulipia nusu gharama za tiketi kwa wageni wote kutoka Mataifa ya Afrika. Mapunguzo zaidi yanapatikana kwa wakazi wa Ukanda wa Afrika Mashariki  au raia wa Tanzania.