ATCL yaanzisha safari mikoa mingine mitano

Muktasari:

  • Ongezeko la vituo hivyo litatoa wigo kwa kila Mtanzania kunufaika na huduma zake hasa baada ya Serikali kuboresha huduma za usafiri wa anga.

Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) linakusudia kuanzisha safari katika mikoa ya Tanga, Musoma, Shinyanga, Iringa na Wilaya ya Mpanda mkoani Rukwa.

Ongezeko la vituo hivyo litatoa wigo kwa kila Mtanzania kunufaika na huduma zake hasa baada ya Serikali kuboresha huduma za usafiri wa anga.

Akiongea jana kwenye maonyesho ya Sabasaba, mkurugenzi mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema kwa sasa wanaendelea na utafiti kwenye viwanja ambavyo ndege zao zitaanza kufanya safari.

“Tunakusudia pia kuongeza safari, badala ya mara moja ndege ziweze kwenda kwa siku mara mbili kwenye baadhi ya maeneo kama Dodoma. Hiyo ni mipango ya kibiashara pengine mpaka mwisho wa mwaka huu tutakuwa tumejua,” alisema.

Akizungumzia ndege mpya, Boeing 787-8 Dreamliner, alisema itakuwa na marubani wanane ambao wote watakuwa ni Watanzania.

“Marubani wanane wa Kitanzania ambao tayari wameshapata mafunzo kwa kushirikiana na wengine ambao waliwasili na ndege hiyo watashirikiana kutoa huduma za awali. Safari ya kwanza itaanzia Dar es Salaam kwenda Mwanza kupitia Kilimanjaro,” alisema.

Pia, aliwaomba Watanzania kuipokea ndege hiyo na kubainisha kuwa zipo mbili nyingine zitaingia mwezi Novemba.

Licha ya Dreamliner iliyowasili Juni 8, ATCL inazo ndege tatu aina ya Bombardier zinazoendelea kutoa huduma.

Kwa sasa ndege za shirika hilo zinatua Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Songea, Tabora, Kigoma, Bukoba, Mtwara pamoja na Visiwa vya Comoro.