Jalada kesi ya vigogo wa uthaminishaji Almasi lipo kwa DPP

Muktasari:

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 94 ya mwaka 2017 niArchard Kalugendo na Edward Rweyemamu wote wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini, wanaoshtakiwa kwa kuisababishia serikali hasara ya Sh2.4bilioni.

Dar es Salaam. Jalada la kesi ya Uhujumu Uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh2.4bilioni, inayowakabili vigogo wawili wa Uthaminishaji wa madini ya Almasi wa Serikali, lipo mikononi mwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kwa ajili ya kulipitia.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya namba 94 ya mwaka 2017 ni Mkurugenzi wa Uthaminishaji madini ya Almasi na vito Tanzania (Tansort) Archard Kalugendo na Mthamini madini ya Almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu.

Akizungumza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Septemba 12 Wakili wa Serikali Sada Mohamed amesema jalada la kesi hiyo lipo kwa DPP kwa ajili ya kulipitia na kulitolea maamuzi.

Sada ameyasema hayo mbele ya  Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Wilbard Mashauri.

"Shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa na jalada la kesi hii, lipo kwa DPP kwa ajili ya kulipitia, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedai Sada.

Baada ya Sada kueleza hayo, Hakimu Mashauri aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 25, mwaka huu itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka linalowakabili kutokuwa na dhamana.

Washtakiwa ambao wote ni waajiriwa wa Wizara ya Nishati na Madini kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja ya uhujumu uchumi katika Mahakama hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kuwa kati ya Agosti 25 na 31, 2017 katika maeneo mbalimbali kati ya Dar es Salaam na Shinyanga, kwa pamoja na kwa vitendo vyao wakiwa wathamini wa madini waliisababishia Serikali, hasara ya 2.4bilioni.