Kauli ya Jenerali Mabeyo yazua jambo bungeni

Monday April 15 2019

 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Mlimba (Chadema) Suzan Kiwanga amehoji Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF) Tanzania, Jenerali  Venance Mabeyo kufanya uchunguzi wa makosa ya uchochezi ni kinyume cha Katiba.

Kiwanga ametoa kauli hiyo bungeni leo Jumatatu Aprili 15, 2019 na kuungwa mkono na  Mbunge wa Mbozi (Chadema) Pascal Haonga.

Wabunge hao walikuwa wakichangia makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais Tamisemi na Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Kiwanga amesema Mabeho alimwambia Rais John Magufuli kuwa aachiwe kazi anachunguza kwa wanasiasa ambao wanatoa kauli ambazo zinaenda kuvunjisha amani .

“Sasa katika utawala bora Serikali nataka nipewe majibu, mkuu wa majeshi wa nchi hii amekuwa DPP (Mwendesha Mashtaka mkuu wa Serikali).”

“Anafanya uchunguzi yeye ni kiongozi anajiingiza kwenye siasa anataka kuingiza nchi  katika matatizo makubwa na ashindwe katika jina la Yesu.”

Hata hivyo, alisimama Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama na kusema kuwa  CDF hakusema kuwa anachunguza wanasiasa.

“CDF alizungumzia masuala ya amani, utulivu na usalama kwa ujumla hakusema wanasiasa naomba tuliweke vizuri jambo hili,” amesema.

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amewataka wabunge kuwa waangalifu wakati wanapozungumzia kauli ambazo hazina uhakika zinazohusu viongozi wengine.

“Tuwe waangalifu kwa sababu mimi nilikuwepo alisema wanafuatilia si wanachunguza kwa hiyo. Sisi wenyewe ni viongozi tunapotaka kuzisema kauli za wengine tuwe na uhakika na kile kilichosemwa,” amesema.

Lakini wakati alipoendelea kuchangia Kiwanga, amesema, “nimekosea lakini kama kufuatilia yeye kwa mujibu wa Katiba anafuatilia  masuala ya watu mbalimbali hapa nchini?”

“DPP atafanya kazi gani kwa kifungu gani cha katiba kinachomruhusu kufuatilia wachochezi  yeye afuatilie mipaka ya nchi.”

Jumamosi iliyopita ya Aprili 15, 2019, katika hafla ya uzinduzi wa mji wa kiserikali uliojengwa Ihumwa mkoani Dodoman ambao ulizinduliwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli, Jenerali Mabeyo alisema Jeshi la Wananchi wa Tanzania linafuatilia kauli tata zinazoashiria uchochezi na kuhatarisha kuibua machafuko ndani ya nchi.

Advertisement