‘Mikataba ya madini kikwazo cha mapato’

Muktasari:

Kwa sasa Serikali imeweka lengo la kufikisha asilimia 10 ya mchango wa madini katika pato la Taifa ifikapo mwaka 2020.

Dar es Salaam. Wadau wa sekta ya madini nchini wamesema mchango wa rasilimali hiyo katika pato la Taifa hautaongezeka kutoka asilimia 3.5 iliyopo sasa ikiwa Serikali haitapitia upya mikataba ya kampuni za madini.

Kwa sasa Serikali imeweka lengo la kufikisha asilimia 10 ya mchango wa madini katika pato la Taifa ifikapo mwaka 2020.

Wakizungumza kwenye mkutano wa kitaifa wa tasnia ya uziduaji uliojadili ufanisi na matumizi bora ya rasilimali kwa manufaa ya umma hivi karibuni jijini Dar es Salaam, baadhi ya wadau hao walisema Tanzania ilijisahau katika uwekezaji wa madini.

Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi alisema mikataba ya kampuni za madini haiwezeshi kujua kiasi cha madini kinachopatikana wakati wa uchimbaji.

Alisema japo kuna mkakati wa uwazi wa sekta ya uziduaji (Eiti), lakini hausaidii kwa sababu unaangalia uwazi wa mapato ya madini baada ya kuuzwa.

“Uchimbaji wa madini ni mnyororo mrefu wa thamani, sisi tunakuja tu kuelezwa huko mbele jinsi walivyouza lakini hatujui tangu wakati wa kuchimba walipata nini. Bado siyo njia sahihi ya kujua mapato yetu ya madini,” alisema Profesa Ngowi.

Mtaalamu wa kodi katika madini, Silas Olang alisema Serikali ilifanya kosa kufuata ushauri wa Benki ya Dunia iliyoshauri kuhusu uwekezaji wa madini katika sera na sheria ili kukaribisha wawekezaji.

Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa aliitaka Serikali kuwekeza kwa wachimbaji wadogo na wa kati ili mapato ya madini yasipelekwe nje na kampuni kubwa za kigeni.

“Serikali inapaswa kuwekeza katika wachimbaji wadogo na wenye leseni za kati ili kipato chao kisaidie ndani badala ya kupelekwa nje ya nchi,” alisema Bashungwa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Kaimu Kamishna wa Madini, John Shija alisema Serikali imetenga Dola 300 milioni za Marekani (Sh6.6 bilioni) kwa ajili ya kuwapa ruzuku wachimbaji wadogo na wa kati ukiwa ni mkakati wa kuwawezesha wazawa katika uwekezaji wa madini.

“Sera ya Madini ya 2009 na Sheria ya Madini ya 2010 zinatutaka kuwapa fursa wachimbaji wadogo na wa kati. Kwa kuwa masharti ya benki na mashirika ya fedha yamekuwa magumu kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo. Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imeanzisha utaratibu wa kutoa ruzuku,” alisema Kamishna Shija na kuongeza:

“Mwaka 2015, Serikali ilitoa Sh7.2 bilioni na mwaka huu tutatoa Dola 300 milioni za Marekani (Sh6.6 bilioni). Tunataka kuzionyesha taasisi za fedha kuwa wachimbaji wadogo na wa kati wanaweza kukopesheka bila ya kuwa na dhamana zisizohamishika na wakalipa.”

Askofu Dk Steven Mangana wa Kanisa la Menonite Tanzania alisema wamekuwa wakiishauri Serikali na kampuni za madini kujenga mazingira bora kwa wachimbaji wadogo na jamii zinazozunguka migodi yao.