Mtoto aliyezaliwa na VVU aishi bila ya virusi kwa miaka minane

Muktasari:

  • Inaelezwa kwamba hii ni mara ya kwanza kwa mtu mwenye VVU kuishi bila virusi hivyo barani Afrika.

Afrika Kusini. Wanasayansi Afrika Kusini wamebaini kwamba mtoto aliyeambukizwa virusi vya Ukimwi, ameishi kwa miaka minane na nusu bila viini hivyo.

Mtoto huyo alipewa dawa za majaribio ya kukabiliana na virusi hivyo alipozaliwa lakini hajapewa dawa zozote za kukabiliana na  virusi hivyo tangu afikishe mwaka mmoja.

Hii ni mara ya kwanza kwa mtu mwenye VVU kuishi bila virusi hivyo barani Afrika.

Wanasayansi waliogundua kuhusu afya ya mtoto huyo mwenye miaka 9 na nusu kwa sasa, wanamuangalia na kumfuatilia kwa karibu zaidi.

Wanasema kuwa matukio kama hayo ni machache na kwamba familia ya mtoto huyo ina furaha.

Watafiti wanaamini kupotea huko kwa vurusi sio kwa sababu ya matibabu lakini mtoto huyo ana jeni ama kinga zisizokuwa za kawaida ambazo zimemlinda dhidi ya virusi vya Ukimwi.