Museveni ana hofu na watu wa nje kuliko Waganda?

Rais Yoweri Museveni wa Uganda.

Muktasari:

  • Matukio yanayompata mwanasiasa kijana wa Uganda Bobi Wine siyo mapya. Yamekuwa yakifanyika nchini humo kwa miaka mingi dhidi ya kiongozi wa upinzani, Dk Kiiza Besigye lakini waganda waliyavumilia.
  • Hivi sasa inaonekana wameonyesha kuchoka na jumuiya ya Kimataifa imewaunga mkono. Hii inaweza kuleta mabadiliko makubwa nchini Uganda.

Tangu ulipofanyika uchaguzi wa mdogo wa kiti cha Mbunge wa Arua Mjini mwishoni mwa Julai na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kuamuru kikosi chake maalumu cha ulinzi kuwashughulikia wanasiasa wa upinzani akiwamo Mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi au Bob Wine inaonekana mambo hayaendi vizuri kwa mtawala huyu wa muda mrefu barani Afrika.

Dunia nzima kupitia vyombo maarufu vya habari kama runinga na mitandao ya kijamii ilijionea namna Bob Wine alivyotendewa sivyo kwa kuteswa na walinzi hao wa rais kwa sababu inaonekana dhahiri kuwa aliteswa vilivyo. Mpaka sasa, licha ya kupokea matibabu kutoka katika hospitali nchini Marekani, bado anachechemea na anatumia magongo.

Kwa bahati nzuri linapokuja suala la kukiuka haki za binadamu na ukandamizaji wa raia wa nchi yoyote na popote pale duniani, linakuwa ni suala la kidunia na kwa hapo hakuna kitu kinaitwa uingiliaji wa mambo ya ndani.

Ulimwengu umekuwa na umoja wa hali ya juu kuhusu kulinda na kuthamini haki za binadamu na suala hilo halina mipaka kwa wanaozivunja kama ambavyo watawala wa bara la Afrika wanataka tuamini.

Watu wakiteswa, kupigwa au kuuawa Kampala, Uganda maumivu yao yanawahusu watu wanaoishi Washington, Marekani na majibu yao kuhusu vitendo hivyo yanakuwa na athari kubwa kwa wahusika ikiwa ni pamoja na kulaaniwa au kufunguliwa mashtaka katika mahakama ya Haki za binadamu iliyoko Uholanzi.

Waganda wamekuwa wakimvumilia Museveni kwa kipindi kirefu na kwa jinsi ambavyo amekuwa akimtendea mpiganaji mwenzake, Dk Kiiza Besigye. Besigye amekuwa mpinzani mkubwa wa Museveni kwa kipindi kirefu lakini madhila ambayo amekuwa akipitia kutoka kwa vikosi vya ulinzi na usalama ni yenye kuhuzunisha sana. Inawezekana kuja kwa mwanasiasa kijana, Bob Wine, mwenye ushawishi mkubwa kutoka katika tasnia ya muziki umeleta chachu mpya ambayo kwa kadri siku zinavyokwenda haitampa usingizi wa pono Rais Museveni licha ya kuwa na vikosi vya ulinzi na usalama tiifu kwake.

Watu wa Uganda wamekuwa wakilalamika kwa jinsi Museveni anavyoendesha utawala wake nchini humo ambao umekuwa kama ufalme wa aina fulani lakini amekuwa hajali.

Alipoingia kwa mtutu wa bunduki na kuchukua utawala wa nchi hiyo mwaka 1986 aliwaponda sana watawala wa Afrika kwa kusema kuwa wanakuwa tatizo pale wanapojikita madarakani kwa muda mrefu na hivyo kufikia mahali ambapo hawawezi kufikiri vizuri namna ya kuondoa matatizo ya watu wao na akiwa na maana kuwa yeye asingeishi muda mrefu katika kiti cha enzi.

Mwaka huo alikuwa kijana na hakuwa na wazo kuwa urais Afrika ni lulu ambayo siyo rahisi kuiacha kirahisi.

Lakini kadri siku zinavyokwenda ameendelea kujiimarisha kukalia kiti hicho kwa kubadilisha vifungu vya katiba na kuweka sheria kandamizi dhidi ya watu wake kiasi ambacho hali imekuwa si himilivu.

Alianza kwa kuondoa ukomo wa vipindi viwili vya urais vya miaka mitano mitano, akaja akaondoa kikomo cha umri ambapo ilikuwa kwa mgombea urais anayezidi miaka 75 hangeweza kushika wadhifa huo.

Rais Museveni amekuwa hatishwi na kuzorota kwa hali ya usalama kwa Waganda ambapo watu wanatekwa na kuuawa mchana kweupe na wengine ni maofisa wakubwa katika jeshi la polisi ambao ndiyo wenye jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao. Wanasiasa nao hawajapona katika uzorotaji huu wa usalama lakini kila kukicha anaishia kutoa kauli za kufanya hili na lile huku hali ikizidi kuwa mbaya kila uchao.

Utawala wake tangu ulipofanikiwa kumwondosha mpiganaji wa siku nyingi wa kikundi cha Lord’s Resistance Army, Joseph Kony kutoka katika ardhi ya Uganda na kukimbilia kwenye misitu ya nchi jirani ya Afrika ya Kati alikuwa amefika mahali ambapo hakuwa na wasiwasi tena kuhusu hali ya ulinzi na usalama nchini mwake lakini kutunishiana misuli kati ya jeshi la nchi hiyo na polisi na kuanzishwa magenge ya utekaji, utesaji na uuaji na askari wasio waaminifu ndani ya jeshi la polisi na hasa kundi linalojulikana kama Bodaboda 2010, limefanya nchi hiyo kuwa katika sintofahamu linapokuja suala la kumjua nani ni nani katika vitendo hivyo viovu.

Miaka ya karibuni kumekuwa na tishio la usalama kutoka kwa kikundi cha Wasomali wenye itikadi kali cha Al Shabab kwa sababu mara kadhaa wamefanikiwa kushambaulia nchi hiyo.

Al Shabab wanapinga serikali ya Uganda kupeleka wanajeshi wake nchini humo kushirikiana na Serikali ya nchi hiyo ambayo wao wanaona imewekwa na mataifa ya magharibi na siyo ya Wasomari wenyewe.

Vilevile kuna makundi ambayo yamekuwa yakifanya mashambulizi yao kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambayo kwa kiasi fulani yamedhibitiwa na serikali ya nchi hiyo.

Waganda wamekuwa wakilalamikia kukua kwa vitendo vya wizi wa fedha za umma na ulaji rushwa ambao umekithiri katika safu ya uongozi ndani ya serikali yake na wateule wake lakini hakuna ambacho kimekuwa kikifanyika kudhibiti hali ya mambo.

Akiwa madarakani amezidi kuimarisha himaya yake kwa kuwaweka watu wa karibu yake kuwa katika kikosi chake cha ulinzi na kumfanya mwanaye Meja Jenerali Muhozi Kainerugaba kuwa mkuu wa kikosi hicho huku wana ndugu na mkewe wakipatiwa uwaziri.

Kwa kujua kuwa Waganda hawana uwezo wa kumwajibisha amekuwa akitamba kuwa yeye yupo katika utawala kwa manufaa yake na familia yake na hata kufikia kusema kuwa Uganda ni sawa na shamba lake la migomba, hivyo anaweza kufanya anachotaka pasipo madhara.

Lakini safari hii inaonekana ameshikwa pabaya hasa baada ya serikali ya Marekani kumpa onyo kwa vile anavyokiuka haki za binadamu na anavyowanyanyasa wapinzani wake.

Kama hiyo haitoshi Bunge la Umoja wa Ulaya, EU lilipokutana wiki hii mjini Strasbourg nchini Ufaransa liliazimia vilevile kumpa onyo na ikiwezekana kusitisha misaada yake kwa Uganda.

Bila kusita Museveni kupitia kwa msemaji wake, Dk Ofyono Opondo alizitaka nchi za kigeni ziache kuingilia mambo ya ndani ya Uganda kwa sababu ni nchi huru na akasema kuwa anao ushahidi wa kuonyesha jinsi mataifa ya ng’ambo yanavyotoa fedha kufadhili upinzani nchi humo.

Museveni kwa sasa amejua hatari inayomkabili kwa sababu yeye mwenyewe aliingia kwa msaada wa nchi za nje na hasa msaada mkubwa kutoka katika nchi jirani za Tanzania na Msumbiji na zile za magharibi ambazo zilikuwa zimechoshwa na utawala wa Iddi Amini na Milton Obote.

Kwa hiyo, nguvu hiyo ya nje ndiyo inayomfanya Museveni kushtuka na hata Bob Wine aliporejea juzi akitokea Marekani kwa matibabu askari wake hawakuonekana wakiwapiga wafuasi wa mbunge huyo ambao walikuwa wanamsubiri na hata mabomu ya machozi tuliyozoea kuyaona hayakutupwa kwa sababu mabwana wakubwa hao walikuwa wakifuatilia kwa karibu hali ya mambo nchini humo.

Museveni anajua kuwa kama mataifa ya nje hasa Ulaya na Marekani yakiamua kumwondoa mtawala yeyote Afrika au pengine duniani hayawezi kushindwa .

Muammar Ghadafi wa Libya ambaye alimsihi Museveni asiondoke madarakani kwa sanduku la kura kwa sababu aliingia kwa mtutu wa bunduki, yeye aliondoshwa kwa nguvu ya madola. Inawezekana kwa Museveni muda wa kumwondosha haujafika kwa sababu inaonekana wakubwa hao hawajawa na mbadala wake. Siku wakiamua ndiyo mwisho wa enzi ya mtawala huyu wa muda mrefu barani Afrika.

[email protected] 0783 165487