Sh19 bil kukarabati miundombinu ya maji

Thursday July 12 2018

 

By Anthony Mayunga, Mwananchi [email protected]

Watu 57,000 watanufaika na mradi wa majisafi na salama

Serengeti. Miundombinu ya maji iliyodumu kwa miaka 44, wilayani Mugumu, Mara, inatarajia kukarabatiwa kwa Sh19 bilioni zilizotolewa na Serikali ya India.

Asilimia 63 ya wakazi 34,000 wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mugumu ndio wanaopata maji ambayo pia si safi na salama kwa kuwa chanzo hakina chujio.

Kaimu meneja wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Mugumu (Muguwasa) Charles Msiba alisema miundombinu hiyo ilijengwa mwaka 1974 na ilikuwa na tanki lenye ujazo wa lita 675.

“Miaka 44 imepita na tangu wakati huo, kumekuwa na ongezeko kubwa la watu na miundombinu imebaki ile ile, hali ambayo imesababisha watu kupata maji kwa mgao na kuifanya Muguwasa kushindwa kujiendesha ikiwamo kuongeza wateja,” alisema Msiba.

Alifafanua kuwa kutokana na changamoto hiyo, wanakusanya ankara kati ya Sh10 milioni kwa mwezi wakati matumizi ya umeme ni zaidi ya Sh13 milioni.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Juma Porini alisema mradi huo utafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo kwa kuwa watakuwa na uhakika wa kuanzisha bustani na shughuli nyingine zinazohitaji maji.

Kuhusu chujio la maji, mkuu wa wilaya hiyo Nurdin Babu alisema naibu katibu mkuu wa wizara ya maji alikuwa wilayani hapo na kuahidi kuwa Serikali itatoa fedha ili mkandarasi aweze kumalizia kazi.

Alisema mpango wa Serikali ni kuhakikisha chujio linakamilika kabla ya mwaka 2019 na zaidi ya Sh2.1 bilioni zitatumika.

Aliongea kuwa zaidi ya watu 57,000 watanufaika na mradi huo.

Chujio hilo lililoanza kujengwa mwaka 2014 lilitarajiwa kukamilika mwaka 2015, hata hivyo, Juni 6, 2017 aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa alimuahidi Makamu wa Rais Samia Suluhu kuwa mradi huo ungekamilika Oktoba mwaka jana.

Advertisement