Uzalishaji maziwa bado duni nchini

Thursday July 12 2018

 

Dar es Salaam. Tanzania bado haijafikia kiwango cha mahitaji ya maziwa yanayotakiwa kuzalishwa kwa mwaka cha lita bilioni 2.6.

Msajili wa Bodi ya Maziwa (TDB), Jeremiah Temu alisema hayo jana katika mkutano wa wadau wa maziwa na kuongeza kuwa kutopatikana kwa kiasi hicho, kunairudisha nyuma sekta ya maziwa. Alisema kwa mwaka 2017/18 lita bilioni 2.4 zilizalishwa ukilinganisha na lita 2.1 bilioni zilizozalishwa mwaka 2016/17.

Temu alisema kwamba mahitaji ya maziwa hapa nchini ni lita 2.6 bilioni jambo linaloonyesha iwapo yote yakifika sokoni yanauzika kwa sababu uhitaji unalingana na uzalishaji.

“Kiwango kinachozalishwa siyo chote kinachokwenda kwa mlaji jambo linalosababisha sekta hii kurudi nyuma endapo vingejengwa vituo vya ukusanyaji ingesaidia kufikisha bidhaa hiyo sokoni,” alisema Temu.

Alifafanua kuwa kwa sasa vipo vituo 180 vinavyokusanya maziwa nchini lakini vinavyofanya kazi ni asilimia 30 pekee.

“Nawasihi wadau wa sekta hii kuwekeza katika ujengwaji wa vituo vya kukusanya maziwa kwa kushirikiana na vyama vya ushirika ambavyo vitahusika katika kuendesha vyama hivyo.

“Takwimu zinaonyesha kuwa kwa mwaka mwananchi mmoja bado anakunywa lita 47 ilhali anatakiwa kunywa lita 200 jambo linaloonyesha unywaji wa maziwa upo chini,” alisema

Advertisement