Veta waja na mashine ya kunyunyiza dawa inayotumia umeme wa jua

Thursday July 12 2018

 

By Kalunde Jama, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (Veta) imebuni mashine ya kunyunyiza dawa kwenye mazao inayotumia umeme wa jua.

Mashine hiyo, ambayo hutumika ikiwa inasukumwa, ina matairi manne na ina mabomba yanayonyunyiza dawa.

Akizungumza katika maonyesho ya 42 ya biashara ya kimataifa (Sabasaba) Mbunifu kutoka Veta Mikumi, Jones Hokororo alisema mashine hiyo ni rafiki kwa mkulima na haimchoshi.

“Mashine hii ni rafiki kwa binadamu kwa sababu haimchoshi na ina uwezo wa kumwagilia eneo kubwa kwa muda mdogo,” alisema Hokororo.

Akielezea namna inavyofanya kazi alisema unaweka dawa ndani ya matenki yaliyoko kwenye bodi ya mashine hiyo kisha unaiwasha na kuanza kuendesha katika shamba huku ikimwaga dawa katika mazao kulingana na mpangilio wa shamba.

“Siku zote tulizoea kuweka dawa katika tenki na kulibeba mgongoni kisha kuanza kupuliza dawa. “Kwa kutumia mashine hii hakuna haja ya kubeba mzigo mgongoni wala kwenda na kurudi mara nyingi kutokana na tenki kuwa na njia moja,” alisema Hokororo.

Alifafanua kuwa wameamua kufunga umeme wa jua kwenye mashine hiyo ili kupunguza gharama kwa sababu inatumia mega wati 50 hivyo kwa kutumia nishati ya umeme wa kawaida itakuwa na gharama kubwa.

Advertisement