Wafanyabiashara wapigwa faini ya Sh24 milioni kwa kubeba madini bila leseni

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kulipa faini ya Sh 24 milioni au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela wafanyabiashara wawili wa madini baada ya  kukiri na kutiwa hatiani kwa  kukutwa na madini aina ya Coloured Gemstones yenye thamani ya dola za Marekani 1.7milioni (Sh4bilioni) bila  leseni.

 

BY Tausi Ally, Mwananchi. tally@mwananchi.co.tz

IN SUMMARY

Wafanyabiashara hao walikutwa na madini aina ya ‘coulored gemstone’ yenye thamani ya Sh4bilioni, bila leseni.

 

Advertisement

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kulipa faini ya Sh 24 milioni au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela wafanyabiashara wawili wa madini baada ya  kukiri na kutiwa hatiani kwa  kukutwa na madini aina ya Coloured Gemstones yenye thamani ya dola za Marekani 1.7milioni (Sh4bilioni) bila  leseni.

Hata hivyo sambamba na adhabu hiyo mahakama ilitoa amri ya kuyataifisha madini hayo.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustino Rwizire amewahukumu washtakiwa hao leo Agosti 12, mwaka huu mara baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande kuwasomea mashtaka mawili yanayowakabili  washtakiwa hao  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na wakayakiri.

Baada ya washtakiwa hao kukiri makosa hayo, Wakili Pande aliiomba Mahakama kuhamia Msasani ambapo vielelezo vya kesi hiyo vipo.

 

Mahakama ilikubali na kuhamia Msasani ambapo kesi hiyo iliendeshwa na washtakiwa kutiwa hatiani na hatimaye kupewa adhabu hizo.

Washitakiwa hao ni  Azam Nazim raia wa India na Ango Mbossa raia wa Tanzania.

Akiwasomea hukumu hiyo, Hakimu Rwizire  amesema alizingatia hoja za wakili wa upande wa Mashtaka Jacqline Nyantori na wakili wa  upande wa utetezi Hudson Ndusyepo.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Rwizire amemtaka kila mshtakiwa kulipa faini ya Sh 6 milioni katika kila kosa au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila kosa.

Kwa kuwa kila mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili hivyo kila mshtakiwa atapaswa kutoa faini ya Sh12 milioni iwapo atashindwa atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa kuwa vifungo hivyo vinaenda sambamba.

 Kabla ya washtakiwa hao kusomewa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Joseph Pande aliiomba Mahakama iwape adhabu kali washtakiwa hao kwa vile nchi inategemea vyanzo vingi vya mapato ikiwemo madini.

Pande pia aliomba Mahakama itoe amri ya kutaifisha hayo madini.

Wakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo yeye aliomba wateja wake wapewe adhabu nafuu kwa kuwa ni wakosaji  wa mara ya kwanza na wamekiri makosa yao.

Ndusyepo amedai kuwa  washtakiwa hao wana wategemezi na kwamba hawakudhamiria kutenda kosa hilo, kwani kosa hilo  limefanyika kwa makosa ya kisheria.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo  kati ya Januari 2017 na Juni 2018 katika maeneo ya Msisiri A eneo la Mwananyamala.

Wanadaiwa kukutwa na madini aina ya Coloured Gemstones kilogramu 75,920.04 yenye thamani ya dola za Kimarekani 1.7 milioni ambazo ni sawa na zaidi ya Sh 4 bilioni bila kuwa na leseni.

Hata hivyo washtakiwa hao wamelipa faini hizo na kukwepa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela.

More From Mwananchi
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept