‘TCRA lindeni maadili ya nchi’
Muktasari:
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa sherehe za ukomo wa utangazaji wa televisheni kwa mfumo wa analojia aliitaka TCRA kusimamia kwa ukamilifu maudhui kwenye vituo vyote vya runinga yanayowafikia wananchi ili yatumike kwa maendeleo .
Dar es Salaam. Makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib Bilal ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuhakikisha kuwa chaneli zote za runinga zinatoa mafundisho yanayoendana na maadili kwa ustawi wa maendeleo ya Taifa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa sherehe za ukomo wa utangazaji wa televisheni kwa mfumo wa analojia aliitaka TCRA kusimamia kwa ukamilifu maudhui kwenye vituo vyote vya runinga yanayowafikia wananchi ili yatumike kwa maendeleo .
“Tuna changamoto ya kutengeneza maudhui ya ndani (Local Content) ili tuweze kutangaza utamaduni wetu ndani na nje ya nchi, kwa sasa mfumo wa dijitali umejaa maudhui mengi kutoka nje,” alisema Dk Bilal.
Alizitaka taasisi husika kushirikiana na wadau wote kutafuta mbinu bora na kutumia fursa ya mfumo huu kutengeneza maudhui yatakayotangaza nchi, utamaduni, kukuza na kuimarisha amani, utulivu na maendeleo.
Alizitaka taasisi za elimu nchini kutoa elimu kwa njia ya runinga ili kurahisisha ufundishaji wa masomo mbalimbali yakiwamo ya Sayansi na Historia.
Alisema anaamini taasisi hizo zikitoa elimu kwa njia hiyo itakuwa rahisi kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja, pia itapunguza gharama za ufundishaji.
Katibu Mtendaji wa Baraza la watumiaji wa mawasiliano nchini, Mary Msuya amesema TCRA itafute teknolojia mpya ya kuepuka uwapo wa utitiri wa ving’amuzi na badala yake itumike kadi moja kwa ving’amuzi vyote.
Mkurugenzi wa TCRA, Profesa John Nkoma alisema Tanzania ina vituo vya runinga 28 na redio 104 lakini kutokana na mabadiliko hayo ni dhahiri idadi itaongezeka.
Alisema changamoto kubwa ni kuhusu bei za vin’gamuzi kwani ya chini ni Sh150,000 jambo ambalo wananchi wa hali duni wanashindwa kuvimiliki na kuhusu matumizi ya king’amuzi kimoja, suala hilo linahitaji maandalizi hivyo litachukua muda mrefu.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa alisema, wakati wanaanza mchakato wa kubadilisha mfumo wa kuhamia dijitali, wananchi walidhani Serikali inawadanganya.
“Tulipozima mitambo hii kwa mara ya kwanza, Rais Jakaya Kikwete alinipigia simu usiku saa moja kuniuliza inakuwaje wananchi wanalalamika hivyo, nikamjibu natekeleza sheria, Rais akasema Profesa endelea na kazi yako nikafurahi sana na leo nimefanikisha,” alisema Makame.