Ukawa wamweka kati Lipumba

Profesa Ibrahim Lipumba

Muktasari:

Wakati Ukawa ikitangaza msimamo huo, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inamtambua kuwa ndiye mwenyekiti halali wa CUF, ametangaza kuwatimua wakurugenzi sita wa chama hicho.

Dar es Salaam. Vyama vitatu vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa); Chadema, NCCR–Mageuzi na NLD vimejitosa rasmi kwenye mgogoro unaokikabili chama mwenza cha CUF, ukisema upo bega kwa bega na kambi inayoongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad.

Wakati Ukawa ikitangaza msimamo huo, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inamtambua kuwa ndiye mwenyekiti halali wa CUF, ametangaza kuwatimua wakurugenzi sita wa chama hicho.

Msimamo wa Ukawa

Katika tamko la pamoja lililotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mbele ya Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia na wa NLD, Oscar Makaidi, umoja huo umesema Profesa Lipumba hana sifa ya kuwa kiongozi wa chama cha upinzani.

“Bwana yule (Profesa Lipumba) mtakumbuka alikimbia chama chake wakati kinamhitaji. Ni kama mzazi anayeikimbia familia yake wakati wa matatizo akitegemea itateketea, halafu ikaibuka vizuri, basi anataka kujisogeza ili kujitambulisha kwa matunda yaliyopatikana CUF chini ya Ukawa,” alisema Mbowe.