RC Arusha anavyosafiria nyota ya Lema kwa JPM

Muktasari:

Wakati Gambo akitarajia kupandishwa cheo na Rais John Magufuli, madiwani wa jiji hilo wametangaza kususia vikao vyote hadi viongozi wa juu wa Serikali watakapoingilia kati mgogoro uliopo.

Arusha. Kama mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema anapambana na Mrisho Gambo ili kujijenga kwa wananchi wake, basi mkuu huyo wa mkoa ananufaika na vita hiyo na anatarajia makubwa zaidi baada ya mzozo wa mwanzoni mwa wiki.

Wakati Gambo akitarajia kupandishwa cheo na Rais John Magufuli, madiwani wa jiji hilo wametangaza kususia vikao vyote hadi viongozi wa juu wa Serikali watakapoingilia kati mgogoro uliopo.

Wawili hao waliingia kwenye mzozo mwingine mapema wiki hii wakati Gambo alipoalikwa kuzindua ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto, itakayojengwa kwa ufadhili wa taasisi ya Martenity Africa alipojaribu kueleza historia ya kiwanja cha jengo hilo, maelezo ambayo Lema aliyapinga kwa sauti kubwa na kusababisha shughuli hiyo kuvurugika.

Baada ya mzozo huo, Gambo amedokeza kuwa kuna makubwa yanafuata.

“Baada ya hilo, simu zilikuja kibao, lakini bahati nzuri kabla sijauliza kokote, na Mheshimiwa Rais ndio akawa ananipigia akaniambia nina full confidence (nina imani) na wewe. Labda wafikirie promotion (kupandisha cheo), lakini hayo mengine hayapo,” alisema Gambo akiwaeleza wafanyabiashara wa mjini hapa kuhusu barua iliyosambaa juzi kwenye mitandao ya kijamii kuwa Rais ametengua uteuzi wake.

“Baadaye (Rais) akaniambia kwamba sasa ili (wafanyabiashara) wajue kwamba kweli nimekupigia simu, niitie mmoja uliye naye karibu ili niongee naye. Ndio (mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Arusha) akapata previledge (bahati) naye ya kuongea na Mheshimiwa Rais.”

Iwapo Gambo atapandishwa cheo, ambacho kwa mukhtadha wa utumishi wa umma chaweza kuwa ni kuteuliwa kuwa mbunge na baadaye waziri, itakuwa ni mara ya pili kupanda cheo siku chache baada ya kuzozana na Lema.

Gambo, ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha Juni 26, alilumbana na Lema Agosti Mosi mbele na Naibu Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jafo.

Katika tukio hilo, Lema alisema Gambo haheshimu mipaka ya kazi zake, akimtuhumu kuingilia maamuzi ambayo tayari yameshajadiliwa kwenye vikao halali vya halmashauri  na kupitishwa na ofisi ya mkuu wa mkoa katika kikao cha  wakuu wa idara, maofisa tarafa, waratibu wa elimu kata watumishi wa Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira (Auwsa)  jijini hapa.

“Nimeona nizungumze hapahapa ili naibu waziri ufahamu hali ilivyo hapa. Kwa mfano Baraza la Madiwani la mwaka 2008, ndilo lililopitisha kiwango cha posho kwa  madiwani kutoka Sh100,000 hadi 120,000. Jambo la kushangaza DC ameandika barua Tamisemi na nakala kwa Takukuru ili wachunguze jambo ambalo limeshapata baraka za Tamisemi,” alisema Lema.

Hali hiyo ilimfanya naibu waziri kuingilia kati na kuahidi kuzishughulikia  changamoto hizo na kumpa nafasi Gambo, ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa wilaya, kujibu hoja hizo. “Mheshimiwa mbunge nataka ujue mimi ndiyo mkuu wa shughuli za Serikali hapa wilayani. Muda wowote nina uwezo wa kuingilia kati mambo ambayo naona hayaendi sawa, hata kama yupo katibu tawala na viongozi wengine,” alisema Gambo.

“Rais aliona ninafaa ndiyo maana akaniteua na sihitaji kujifunza namna ya kuwa mkuu wa wilaya huu kwa kuwa ni mwaka tano.”

Malumbano hayo yaliendelea na kumuhusisha pia Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ambaye aliungana na Lema na madiwani wengine kupinga jambo hilo.

Baada ya vuta nikuvute hiyo mbele ya waziri, Agosti 18 Gambo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuchukua nafasi ya Felix Ntibenda.

Siku chache baada ya uteuzi huo, Gambo aliagiza halmashauri ya jiji kutafuta fedha za kupunguza deni la walimu ambalo ni Sh154 milioni. Mkurugenzi wa jiji hilo, Athuman Kilamia alitangaza posho za madiwani ambazo zilikuwa zinalipwa kinyume cha taratibu, zitumike kupunguza deni la walimu na zikatolewa.

Mgogoro ukaibuka kati ya madiwani wa jiji hilo ambao wengi ni kutoka Chadema.

Sakata la Jumanne wiki hii linaweza kumpa cheo kikubwa zaidi kutokana na Rais Magufuli kumpigia simu kwa lengo la kumthibitishia kuwa yuko pamoja naye siku ambayo barua ya kughushi ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa mkuu huyo wa nchi ametengua uteuzi wa Gambo.

Sakata hilo lilitokea katika uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto jijini Arusha ambao utagharimu Sh9 bilioni, sehemu kubwa ya fedha hizo zikitoka taasisi ya Martenity Africa.

Mvutano huo ulianza baada ya Gambo kusema kuwa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa hospitali imetolewa na Taasisi ya Mawalla Fund kwa kuwa muasisi wake, Nyaga Mawalla alikuwa na maono ya kusaidia afya ya mama na mtoto.

Kauli yake ilikuwa ikimaanisha kuwa Mfuko wa Maendeleo wa Arusha (ArDF) haikutoa kiwanja hicho kwa Martenity Africa wala kutafuta mfadhili.

Jambo hilo liliwakera viongozi wa ArDF, ambayo imeanzishwa na Lema na Elifuraha Mlowe, ambaye ni mwenyekiti. Lema alimtaka ndugu wa wakili huyo amsahihishe Gambo, lakini hakuna kilichofanyika, ndipo aliposimama na kuanza kupinga kwa sauti maelezo ya Gambo.

Lema alikuwa akisema mkuu huyo wa mkoa anapotosha ukweli kwa misingi ya kisiasa, kwa kuwa Mawalla Fund ilitoa kiwanja hicho kwa ArDF, ambayo ilitafuta wafadhili na kusaini nao mkataba wa ujenzi wa hospitali.

Wageni kwenye hafla hiyo iliyofanyika Bulka walijaribu kuwatuliza wawili hao, hawakufanikiwa kutokana na Lema kuendelea kueleza kwa sauti kuwa Gambo anapotosha, huku mkuu huyo wa mkoa akizungumza kwenye kipaza sauti kumtaka mbunge huyo atulie.

Shughuli hiyo ilimalizika kiutata na hivyo waandaaji wakashindwa kuendesha harambee iliyopangwa kufanyika baada ya uzinduzi.

Alipoulizwa kuhusu mawasiliano ya Rais na Gambo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa alisema kama Gambo amelisema mwenyewe, itakuwa sahihi.

Mtazamo wa Lema

Akizungumzia sakata hilo, Lema alisema kuwa mteule huyo wa Rais amekuwa na malumbano na yeye mara kadhaa na baadaye kupanda cheo.

“Najua hata katika mgogoro huu wa sasa Gambo anaweza kupandishwa cheo kwa kudhani ananidhibiti mimi, lakini hatutakubali kuvunja utu wetu,” alisema Lema.

Wadau watoa ushauri

Watu waliozungumza na gazeti hili kuhusu sakata hilo walikuwa na maoni tofauti.

“Mgogoro wa RC na Lema ni sehemu tu ya picha nzima,” alisema Richard Mbunda, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Lakini tumesikia mvutano kati ya wateule wa Rais kama wakurugenzi, wakuu wa wilaya na madiwani. Mvutano huu unadumaza morali ya kulitumikia Taifa na uratibu wa mipango ya kimaendeleo kwa wanaoona wanaonewa na hata utengamano wa kijamii, ukizingatia wengine ni wawakilishi wa wananchi.”

Aliwataka wateule wa Rais kumaliza tofauti za kisiasa na viongozi wa vyama vingine badala ya kutumia madaraka yao kibabe.

“Wateule wa Rais wanapungukiwa hilo mkoani Arusha. Si sifa nzuri ya uongozi kuwaweka wawakilishi wa wananchi ndani kwa kuwa tu una mamlaka hayo, kabla hata ya kujaribu kukaa na kuongea nao,” alisema Mbunda akirejea matukio kadhaa ya wakuu wa mikoa na wilaya kuamuru polisi wakamate wanasiasa na kuwaweka ndani.

Mmoja wa wanasiasa wakongwe nchini, Njelu Kakasa alisema kinachoendelea sasa ni wateule wa Rais kutoheshimu viongozi waliochaguliwa na wananchi.

“Viongozi wa kuchaguliwa ni wawakilishi wa wananchi ambao ndiyo wenye mamlaka ya mwisho katika Taifa. Kumkamata kiongozi aliyechaguliwa ni hatari. Ili kuwaheshimu lazima washirikishwe katika shughuli za Serikali,” alisema Kasaka.

Kasaka ambaye aliwahji kuwa mbunge wa Lupa, alisema mzozo wa Gambo na Lema umedhihirisha kuwa bado CCM haijakubali uwepo wa mfumo wa vyama vya upinzani nchini. “Vinginevyo lazima tuwaheshimu viongozi waliochaguliwa na wananchi na tuwape fursa ya kufanya kazi. Serikali iwashirikishe. Hata kama wanatoka vyama vya upinzani, ni viongozi waliochaguliwa na wananchi,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana aliwataka viongozi hao kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuwapelekea wananchi maendeleo.

Dk Bana pia alisema kila kiongozi alipaswa kuangalia mipaka ya mwenzake na kuongeza kuwa Gambo yuko juu kwa cheo kuliko Lema hivyo alipaswa kuheshimiwa.

“Kila mtu anapaswa kuelewa mamlaka ya mwenzake. Mkuu wa Mkoa yuko juu ya mbunge, kama walitaka kuongea kwa kupokezana walipaswa kukutana kwanza na kujadiliana na hata kupanga ratiba kabla ya kwenda hadharani,” alisema Dk Bana.

Madiwani wasusia vikao

Katika hatua nyingine, madiwani wa Jiji la Arusha jana wametangaza kususia vikao vyote hadi hapo viongozi wa juu wa Serikali watakapoingilia kati kumaliza mgogoro baina yao na Gambo.

Lema, akiwa pamoja na madiwani 24 kati ya 25, alitangaza uamuzi huo juzi jioni baada ya kikao cha Kamati ya Mipango ya Jiji kushindwa kufanyika kutokana na wakuu wa idara kutohudhuria na hivyo wajumbe kuona hawatapata majibu sahihi.

“Tumeamua kuanzia sasa hatutakutana tena. Tunajiandaa kwenda Dodoma kuonana na Waziri na Katibu Mkuu wa Tamisemi ili kuwaeleza hali hii,” alisema.

Lema alisema ni bora Baraza la Madiwani livunjwe na kurudia uchaguzi, kwa kuwa haiwezekani madiwani kukaa vikao kupanga mambo ya maendeleo na kukwamishwa na mkuu wa mkoa.

Mwenyekiti wa kamati ya madiwani ya mipango miji, Paul Mathysen alisema kikao hicho kimevunjika kutokana na wakuu wa idara kushindwa kutoa majibu katika hoja za nyuma na kuwataka kujadili mambo mapya. “Mambo yote yamesimama Jiji la Arusha. Tulikuwa na operesheni za usafi zimesimama, tulikuwa na mikakati ya ujenzi mji wa kisasa na mingine mingi imesimama kutokana na migogoro isiyo na sababu,” alisema.

Meya wa Jiji, Calist Lazaro alisema bila viongozi wa juu kutumia busara Arusha haiwezi kutulia kwa kuwa maagizo ya kuliongoza yanatoka nje ya mkurugenzi na baraza la madiwani. “Hata mkurugenzi wangu sasa ninamuonea huruma. Amechanganyikiwa hajui afanye lipi. Naungana na madiwani kuwa hakuna haja ya kufanyika vikao kama hakuna utekelezaji wa maazimio ya madiwani,” alisema.

Calist alisema wakati madiwani wana kikao hicho, wakuu wa idara walikuwa na kikao na mkuu wa mkoa na wafanyabiashara, jambo ambalo alisema si sahihi.

“Kikao hiki alipaswa kuwepo. Ofisa mipango miji alipaswa kuwepo, ofisa ardhi, ofisa afya na wengine lakini wote wameitwa na mkuu wa mkoa. Sasa hatuwezi kufanya kazi katika mazingira haya,” alisema Lazaro. Gambo alikutana na wafanyabiashara hao katika mfululizo wa vikao vyake vya kusikiliza kero za makundi mbalimbali ya kutoa maeleko kwa vyombo vingine vya Serikali kutatua kero hizo.

Baadaye mchana alifanya mkutano wa hadhara katika Kata ya Terrati, kusikiliza kero za wananchi na alitoa lita 600 za mafuta ili kusaidia ukarabati wa barabara eneo hilo.

Mkuu huyo wa mkoa pia aliagiza Mamlaka ya Maji Safi na Taka Arusha (AUWSA) na Shirika la Umeme (Tanesco) kupeleka umeme eneo hilo ambalo kwa sasa lina idadi kubwa ya watu lakini halina maji na umeme. Katika mkutano huo, Gambo pia alimuagiza mkurugenzi wa jiji kuongeza mtumishi wa afya katika kituo cha afya cha Terati na pia kutengeneza ndani ya wiki mbili gari la dharura kwa ajili ya kituo hicho. Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Athuman Kilamia  alipotakiwa jana kuelezea malalamiko ya madiwani alisema alikuwa na taarifa za kikao cha madiwani lakini hana taarifa za maandishi ya mgomo wa madiwani.

“Kama madiwani wana malalamiko wanapaswa kuniandikia badala ya kwenda huko Dodoma kuonana na Waziri wa Tamisemi,” alisema Kilamia.