Askari wanne wadakwa na Takukuru wakidaiwa kupokea rushwa

Muktasari:

Walidaiwa kupokea Sh5milioni ili waiachie mifugo ya familia saba

 Kiteto. Askari wanne wa pori la akiba la Mkungunero Wilaya ya Kondoa Mkoa wa Dodoma wanashikiriwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakituhumiwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh5 milioni za wafugaji wa Kijiji cha Irkiushiboir Kata ya Makame Wilaya ya Kiteto mkoani Mnyara.

 Akizungumza na MCL Digital leo Jumanne Mei 22, 2018 Kamanda wa Takukuru wilayani Kiteto, Julius Chacha amesema askari hao wamekamatwa Mei 20, 2018 wakiwa na bunduki nne aina ya SMG huku wakiwa na mifugo 200.

 Amewataja askari hao kuwa ni  Godfrey Matheas, Martenus Mahoka, Augustino Sadiki na Aphrahimu Polepole.

 Amebainisha kuwa baada ya mmoja wa wafugaji  kuombwa  rushwa na watu hao, uliwekwa mtego na kukamatwa askari hao wakiwa wamepokea kiasi hicho cha fedha na kwamba walikuwa na mifugo zaidi ya 200 mali ya familia saba za wilayani Kiteto.

 “Mtego huo uliwekwa kabla ya askari hao kuikabidhi mifugo kwa wenyewe. Tuliwakamata  wahusika wakiwa wameshikilia mifugo hiyo katika kitongoji cha Ilchura kijiji cha Irkiushiboir wilayani Kiteto,"amesema  Chacha.