Kunguru wasababisha ndege kutua kwa dharura Mombasa

Muktasari:

Polisi wa Viwanja vya Ndege, Mombasa amesema hakuna abiria aliyejeruhiwa. 

Dar es Salaam.  Ndege ya Shirika la ndege la Ujerumani, Condor, imelazimika kutua kwa dharura katika uwanja wa ndege wa Moi, Mombasa, Kenya, baada ya kunguru wawili kuingia katika injini ya ndege hiyo.

Tukio hilo limetokea dakika chache baada ya ndege hiyo kuondoka visiwani Zanzibar, leo Mei 29, saa 3 asubuhi.

 Kwa mujibu wa gazeti dada la Mwananchi, Bussiness Daily, kunguru wawili waliingia kwenye injini ya ndege hiyo.

Polisi wa Viwanja vya Ndege, Pwani, Noah Mviwanda amesema ndege hiyo ilitua salama katika uwanja wa ndege wa Moi, na hakuna abiria yeyote aliyejeruhiwa.
Wakati wanahabari wa Bussiness Daily walipotinga uwanjani hapo, abiria wa ndege hiyo walikuwa wakielekea hotelini.

 Mmoja wa abiria ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema, wataondoka kwa kutumia ndege nyingine, kesho.

 Abiria mwingine, Morris, amesema: “Tunamshukuru Mungu tupo salama, tunakwenda hotelini, hadi kesho tutakaposafiri kwa ndege nyingine.”