Samaki anayezaa badala ya kutaga awa kivutio Sabasaba

Muktasari:

Samaki huyu huishi kwenye kina kirefu cha maji kati ya mita 50 hadi 200 ambapo sio rahisi kufikika.

Dar es Salaam. Samaki aina ya Silikanti ambaye huzaa badala ya kutaga mayai, yuko katika orodha ya viumbe walio hatarini kutoweka duniani.

Samaki huyu huishi kwenye kina kirefu cha maji kati ya mita 50 hadi 200 ambapo sio rahisi kufikika.

Samaki huyo ameonyeshwa leo Julai 5 wakati wa maonyesho ya 42 ya kimataifa ya biashara, maarufu Sabasaba yanayoendelea jijini hapa.

Akizungumza leo, Julai 5 Mhifadhi wa Utalii wa eneo la Silikanti, Tanga David Mtopwa, amesema samaki wa aina hiyo alipotea kwa muda mrefu na sasa ameonekana.

"Samaki huyu ni wa ajabu kwanza anazaa hatagi mayai, maana yake anatotolesha mayai yakiwa tumboni na kutoa vifaranga, wakati samaki wengine hutaga mayai nje kwenye maji hata akivuliwa bahati mbaya huwa haliwi kwani ana mafuta mengi sana," amesema Mpotwa

Ili kumlinda kiumbe hai huyo, serikali ilianzisha hifadhi ya Silikanti kwa lengo la kulinda mazalia yake.

Kwa mara ya kwanza nchini Tanzania alionekana katika eneo la Songo Mnara Kilwa mwaka 2003.

Amesema mwaka 2004 alivuliwa eneo la Kigombe na kwa muda mfupi wa miezi kumi na mbili walivuliwa samaki aina hiyo zaidi ya 37, idadi kubwa kuvuliwa ndani ya muda mfupi.

“Samaki huyu anapatikana nchini Tanzania kwa wingi kupita sehemu nyingine duniani. Watafiti kutoka nchi mbalimbali wanaendelea na kutafiti ili kubaini kwa nini samaki huyo alipotea kwa muda mrefu pamoja na kujua tabia zake ambazo bado hazijajulikana kwa undani,” amesema

Kwa sasa samaki huyo ni kivutio kwa watalii na wengi kwani hupenda kutembelea eneo hilo na kutaka kujua historia yake.