Kairuki awapa kazi Suma-JKT kujenga vituo 7

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki

Muktasari:

Alitoa agizo hilo baada ya katibu mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila kutia saini mkataba wa ujenzi wa vituo hivyo utakaotekelezwa na Suma- JKT.

Dodoma. Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ameliagiza shirika la Suma-JKT kukamilisha kwa wakati ujenzi wa vituo saba vya umahiri, vitakavyotumika kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo.

Alitoa agizo hilo baada ya katibu mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila kutia saini mkataba wa ujenzi wa vituo hivyo utakaotekelezwa na Suma- JKT.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni Mei 31, Kairuki alisema ujenzi wa vituo hivyo utakuwa na manufaa kwa wachimbaji wadogo.

Waziri huyo alisema ujenzi utagharimu Sh11.97 bilioni na utaanza mwezi huu na kukamilika Desemba. “Tuliwapa nafasi Suma- JKT tukiamini hamuwezi kutuangusha, tumeokoa Sh249.3 milioni ukilinganisha kama tungetoa zabuni kwa wengine, msitufanye tujute,” alisema Kairuki.

Naye mkurugenzi mwendeshaji wa Suma-JKT, Morgan Nyonyi alisema mkataba waliopewa ni wa miezi sita, hivyo watafanya kazi kwa nguvu zote lakini kwa weledi wa hali ya juu.

Nyonyi alisema wana nguvu kazi ya kutosha katika kazi hiyo na wamejizatiti kuikamilisha kwa wakati, ikibidi kabla ya muda huo.

Awali, Profesa Msanjila alisema vituo hivyo vitajengwa Bariadi, Musoma, Chunya, Songea, Mpanda na Handeni. Pia, ujenzi wa jengo katika chuo cha madini Dodoma.