Kesi ya Wema mbivu, mbichi kujulikana Ijumaa

Wema Sepetu

Muktasari:

Hukumu hiyo ilipaswa kusomwa jana lakini ilisogezwa hadi Julai 20 kutokana na hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Thomas Simba anayesikiliza shauri hilo kutokamilisha kuandika hukumu.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Ijumaa wiki hii kutoa hukumu ya kesi ya matumizi ya dawa za kulevya inayomkabili msanii na mlimbwende wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu na wafanyakazi wake wawili.

Hukumu hiyo ilipaswa kusomwa jana lakini ilisogezwa hadi Julai 20 kutokana na hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Thomas Simba anayesikiliza shauri hilo kutokamilisha kuandika hukumu.

“Naomba mniwie radhi kuna vitu vichache sijaviweka katika hukumu yangu, hivyo naomba kuiahirisha hadi Julai 20 ili niweze kuvikamilisha,” alisema Simba.

Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa baada ya mawakili wa upande wa utetezi, Albert Msando na wa mashtaka, Costantine Kakula kuwasilisha hoja za majumuisho.

Tayari, mashahidi watano wa upande wa mashtaka wametoa ushahidi na mahakama iliwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu na walianza kujitetea.

Mbali na Wema, washtakiwa wengine ni wafanyakazi wake; Angelina Msigwa (23) na Matrida Abas (19).

Awali, Wema alikubali nyumbani kwake kulikuwa na msokoto unaodhaniwa ni bangi jikoni, vipisi ambavyo hajui ni kitu gani katika chumba cha kuhifadhia nguo zake, pochi, viatu na kiberiti katika chumba wanacholala wanamuziki wawili Jodarn na Mila.

Akiongozwa na Msando kujitetea, Wema alieleza kuwa yeye hajui mmiliki wa vitu hivyo kwa sababu yeye ni msanii wa filamu na nyumbani kwake wanaingia watu tofauti tofauti.

Alidai kawaida huwa anafanya sherehe na kualika watu katika nyama choma na chakula cha mchana.