VIDEO: Waliofariki dunia ajali ya kivuko wafikia 126, miili 36 yatambuliwa

Muktasari:

Idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichozama jana mchana Septemba 20, 2018 imefikia 126 huku uokoaji ukiendelea

Dar es Salaam. Idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichozama jana mchana Septemba 20, 2018 imefikia 126 huku uokoaji ukiendelea.

Akizungumza wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) leo saa 10:30 jioni,  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Issack Kamwelwe amesema miili 37 tayari imetambuliwa na ndugu na jamaa wakati kazi ya kuitambua iliyosalia ikiendelea.

Amesema hadi leo mchana waokoaji walikuwa wameipata miili 76 na waliporejea tena kuanzia saa 10 jioni walifanikiwa kupata mingine na kufanya idadi yake ifikie 126.

Leo saa 5 asubuhi, ilielezwa kuwa miili iliyokuwa imepatikana hadi muda huo ilikuwa 42, jana ilipatikana 44 na kufanya idadi yake kufikia 86, baadaye mchana kuongezeka hadi 94.

Waziri huyo ameahidi kutoa taarifa nyingine saa 12 jioni ambayo itatoa mwelekeo halisi kama kazi ya kuopoa miili mingine itaendelea au kuahirishwa hadi kesho.

“Bado kazi ya kusaka miili zaidi inaendelea. Nitazungumza tena baadaye jioni na tutaeleza  kama tunaweza kuendelea na kazi hii au itatubidi kuahirisha hadi kesho,” amesema.

Hata hivyo, leo mchana Kamwelwe wakati akihojiwa na TBC amesema uokoaji utasitishwa saa 12 jioni.

Kuhusu uokoaji, amesema wazamiaji hawajakumbana na ugumu wowote zaidi ya kukuta mizigo ambayo hulazimika kuitoa kwanza ili waweze kutoa miili.

Kamwelwe amesema kila wakati wamekuwa wakiwasiliana na  na Rais John Magufuli ambaye amekuwa akifuatilia tukio hilo kwa ukaribu mkubwa.

“Mheshimiwa Rais macho yake yote yako huku na kila mara nimekuwa nikiwasiliana naye,” amesema.