Wakulima wa kahawa Kilimanjaro, Arusha walia gharama za pembejeo

Muktasari:

Wakulima wa kahawa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, wameiomba Serikali kusaidia kupatikana unafuu wa pembejeo ili waweze kumudu kuendelea na kilimo cha zao hilo.

Arusha. Baadhi ya wakulima wa kahawa katika maeneo ya mkoa wa Arusha na Kilimanjaro, wameiomba Serikali kuingilia kati ili wapate punguzo la dawa na usaidizi wa maofisa ugani ili kuokoa kudhoofika kilimo cha zao hilo.

Wakizungumza na Mwananchi jana, wakulima hao walieleza gharama kubwa za madawa, kupunguza usaidizi wa maafisa ugani kama Serikali isipoingilia kati kuwasaidia watashindwa kuendelea na kilimo hicho.

Richard Mushi mkazi wa kijiji cha Kyeeri kata ya Machame Magharibi, alisema gharama kubwa za pembejeo zinawafanya kushindwa kupambana na wadadu waharibifu katika kahawa.

"Hivi sasa mfuko wa dawa ya kuua wadudu ni Sh65,000 na bado bei tunayouza kahawa kwenye vyama vya msingi ni Sh2,000 hivyo kwa eka moja unaweza kutumia mifuko 10 ambayo ni sawa na Sh650,000 na ukivuna unaweza kupata kilo 100 ambazo ni Sh1 milioni hivyo ukitoa na gharama nyingine ni hasara," alisema.

Simboufoo Munisi ambaye ni mwanachama wa kikundi cha Wabokati alisema, hali ya kilimo hicho ni ngumu kwani mdudu aina ya bohora amevamia mashamba mengi na kuharibu miche lakini wanakosa usaidizi mzuri wa maafisa ugani.

"Hapa tulikuwa na kiwanda cha kumenya kahawa tumekifunga kwani hali si nzuri na baadhi yetu wameanza kuondoa kahawa shambani na kulima nyanya," alisema.

Joseph Mungure mkulima eneo la Akeri Arumeru alisema wakati Serikali ikihangaikia kupata suluhu ya soko la kahawa ni vyema lkasaidia kwanza vyama vya ushirika viwe na uwezo kununua kahawa yao kwa bei nzuri na kutoa mikopo ya pembejeo.

Hata hivyo, mkurugenzi wa maendeleo ya kahawa na uendeshaji wa bodi ya kahawa nchini (TCB), Kajiru Kisenge alisema changamoto za wakulima kupata pembejeo na huduma za ugani zinashughulikiwa katika ngazi ya halmashauri.

Alisema bodi hiyo inaendelea kujitahidi katika uratibu mzuri wa minada ya kahawa ili wakulima wapate bei nzuri na hivyo kuweza kugharamia pembejeo na mahitaji mengine.

Alisema kutokana na utaratibu ulioanza mwaka huu wa wakulima kutakiwa kuuza kahawa yao kwenye vyama vya msingi na ushirika kabla ya kufikishwa mnadani ambapo kuna wafanyabiashara, inatarajiwa kurahisisha kupatiwa huduma mbalimbali za ugani kwa kuwa watakuwa kwenye vikundi.