Bongo Movie, Bongo Fleva wamuaga Pancho Latino

Muktasari:

Msiba wa mtayarishaji wa muziki Pancho Latino umewakutanisha wasanii na watayarishaji wa zamani na sasa wa muziki wakati wa shughuli za kuuaga mwili wake katika hospitali ya Jeshi Lugalo.


Dar es Salaam. Wasanii na watayarishaji wa muziki wa Bongo Fleva wamejitokeza katika ibada ya mazishi ya  mtayarishaji wa muziki nchini, Joshua Magawa 'Pancho Latino',

 

Ibada hiyo ilifanyika hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Salasala kuanzia saa 4:00 asubuhi na baadaye mwili kusafirishwa kwenda  kijijini kwao Msingisi wilayani Gairo mkoa wa Morogoro ambapo utazikwa kesho.

 

Pancho alifariki Septemba 9 akiwa anapatiwa matibabu katika zahanati ya Mtongani Kunduchi jijini Dar es Salaam baada ya kuzama kwenye maji kwenye kisiwa cha Mbudya.

 

Miongoni mwa waliojitokeza kwenye shughuli ya kuaga jana ni pomoja Mbunge wa Mikumi ambaye pia ni msanii, Joseph Haule 'Profesa Jay', Juma Musa 'Jux',  Amber Lulu, Shetta, Inspekta Haroun, Feruzi, Suma G, Ben Pol, Edu Boy na Wakazi.

 

Wakati kwa upande wa watayarishaji muziki, alikiwapo Akili The Brain, Lamar, G Love na Hanscana.

 

Wakimzungumzia Pancho kwa nyakati tofauti watayarishaji hao akiwamo Akili, walisema marehemu alikuwa ni mtayarishaji aliyekuwa anaheshimu na kujali kazi yake.

 

Lamar alisema Pancho alikuwa mtayarishaji wa kizazi chao baada ya kile cha kina Master Jay kupita na alikuwa na mipango mingi ya kuipeleka sanaa hiyo mbele.

 

Alisema ni mtayarishaji ambaye muziki wake ulikuwa upo katika hadhi ya watayarishaji wa nchi za nje walioanza kazi hiyo muda mrefu.

 

Benpol alisema Pancho tofauti na watayarishaji wengine, alikuwa na ladha tofauti za muziki jambo lililompa uwanda mpana wa kufanya kazi yake.

 

"Kuna mtayarishaji unaweza kusikiliza nyimbo zake tano ukamjua ni nani, lakini sio kwa Pancho alikuwa na ladha tofauti tofauti kwa kweli tumempoteza mtu muhimu kwenye tasnia,” alisema Ben Pol.

 

Naye msanii wa filamu, Kulwa Kikumba 'Dude' alisema Pancho hakuwa msaada kwa wasanii wa muziki tu, bali hata wa filamu kwani amewahi kutengeneza 'sound track' za filamu nyingi ambapo yeye alimjua kupitia Dully Sykes wakati akifanya kazi studio za Dhahabu Records.